Wazazi lindeni watoto wakati wa sikukuu
Wakati zimebaki siku chache kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao kwa kuhakikisha wanakuwa salama, ili kuwaepusha na hatari zinazowakabili.
Sherehe hizi hazipaswi kuwafanya wazazi ama walezi kusahau wajibu wao, kwamba wanatakiwa kuhakikisha watoto wanakuwa salama, ili kuwaepusha na hatari zinazoweza kuharibu sikukuu.
Inafahamika kuwa kipindi hiki cha mapumziko, mwingiliano wa wanafamilia huongezeka, hivyo uangalizi kwa watoto uzingatiwe, kwani kunakuwapo watu wenye kutambua umuhimu wao na wasiotambua ambao huwafanyia vitendo viovu.
Taarifa mbalimbali zimekuwa zikibainisha kuwa wanaowatendea watoto uovu, ikiwamo ubakaji na unyasasaji wa kijinsia, ni wanafamilia au watu wa karibu, hivyo kwa mchanganyiko wa likizo na shamrashamra za sikukuu wanapaswa kupewa uangalizi wa kipekee.
Mbali na hilo, pia kuwe na muda maalumu wa watoto kupumzika, kwani pamoja na sikukuu ni wakati wao wa kupumzika, hivyo badala ya kufuata mkumbo wa matembezi yasiyokwisha ya wageni au wenyeji kwenye familia, watoto watengewe muda wa hilo.
Katika shamrashamra za sikukuu, watoto waangaliwe wanakwenda maeneo gani na kunafanyika nini, ikiwezekana waambatane na watu wazima kuwaepusha na changamoto wanazoweza kukumbana nazo.
Mfano, wanapokwenda kwenye fukwe kuogelea mara kadhaa hutokea matukio yanayogharimu maisha yao, hivyo si tu kuongozana na watu wazima, bali wawaangalie kwa ukaribu zaidi kila wanachofanya.
Tunatumia fursa hii kuwakumbusha na kuwasisitiza wazazi na walezi kuwalinda watoto na kuhakikisha maeneo wanayotembelea ni salama, ili kufurahia sikukuu bila hofu ya kupatwa na madhara yoyote.
Wazazi waepuke kuwaacha watoto peke yao, hasa katika maeneo yenye watu wengi kama masoko, maeneo ya burudani na hata kwenye kumbi za michezo.
Pia watoto waelimishwe jinsi ya kutambua watu wasiowajua au maeneo hatarishi kwa sababu mazingira wanapocheza yanaweza kuwa na athari kwa usalama wao.
Kwa wale watoto wadogo wasiruhusiwe kutoka peke yao, bali waongozane na mtu mzima kwa ajili ya kuwaangalia kwa karibu wasipatwe na madhara.
Katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali, ni muhimu watoto kufahamu namba za simu za wazazi au walezi wao, kwani itawasaidia wanapokutana na dharura, hasa ikiwa wametoka peke yao iwe rahisi kuwasiliana nao.
Pia, watoto wafundishwe jinsi ya kutambua watu wasiowajua au mazingira yanayoweza kuwa hatarishi. Elimu hiyo inapaswa kusisitiza umuhimu wa kuwa waangalifu na kuripoti hali zisizo za kawaida mara moja.
Pamoja na hayo, imezoeleka kuwa nyakati za sikukuu mara nyingi huambatana na safari za kifamilia, michezo, na shughuli mbalimbali zinazofanya watu kuwa mbali na makazi yao kwa muda mrefu, hivyo kuongeza hatari ya wizi au uharibifu wa mali. Tunatahadharisha familia kulinda makazi yao kwani ni jambo muhimu.
Hakikisheni mali muhimu kama fedha taslimu, vyombo vya thamani, au nyaraka muhimu zimehifadhiwa mahali salama.
Kama hakuna ulazima wa wanafamilia wote kuondoka, ni vizuri wakabaki watu wachache nyumbani ili kuhakikisha nyumba inaendelea kuwa salama wakati wote.