Wazazi, walezi wasikwepe jukumu la malezi

Wazazi, walezi wasikwepe jukumu la malezi

Muktasari:

  • Miongoni mwa habari zilizoandikwa na gazeti la Mwananchi la Julai 17, 2021 ni kisa cha mzazi wa mtoto wa miaka 15, Anastasia Dastani ambaye mwanawe alijiingiza kwenye uhalifu na kufanya jaribio la kutaka kumuua kwa kumuwekea sumu kwenye mboga.

Miongoni mwa habari zilizoandikwa na gazeti la Mwananchi la Julai 17, 2021 ni kisa cha mzazi wa mtoto wa miaka 15, Anastasia Dastani ambaye mwanawe alijiingiza kwenye uhalifu na kufanya jaribio la kutaka kumuua kwa kumuwekea sumu kwenye mboga.

Mtoto huyo pia anadaiwa kushiriki matukio ya wizi kwa kuingia madirishani katika nyumba za watu na kuiba vitu anavyovikuta na kuwapa wenzake anaoongozana nao wakiwemo watu wazima wanaomtumia.

Matukio ya watoto kufanya au kufanyiwa vitendo vya kihalifu, ukatili na kuuawa yamekuwa yakishamiri siku hadi siku, huku sababu kubwa ikitajwa ni wazazi kutokuwa karibu na watoto wao.

Wazazi au walezi wengi siku hizi inaelezwa hawatengi muda wa kuzungumza na watoto wao au hawafuatilia maendeleo yao iwe shuleni au nyumbani.

Jukumu la malezi hivi sasa limeachwa kwa walimu au dada wa kazi, ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiwalea kulingana na utashi wao na mazingira waliyonayo.

Tunaamini kuwa jukumu kubwa la malezi ni la mzazi au mlezi; huyu ndiye mwenye kumfanya mtoto awe na tabia nzuri au mbaya. Ndiye wenye uwezo wa kurekebisha kwa urahisi mwenendo usiofaa.

Shughuli za utafutaji mali zisiwaondolee wazazi na walezi wajibu wa ulezi kwa watoto wao ambao wanahitaji malezi yao. Limekuwa jambo la kawaida kwa baadhi ya wazazi kutoonana na watoto wao hadi Jumamosi au Jumapili licha ya kuishi nyumba moja.

Wazazi na walezi wengi hawajui watoto wao wamekula nini, wamevaa nini, wamesoma nini, wana matatizo gani, wanapenda au hawapendi nini. Mambo haya yote wanaweza kuyajua kama watakuwa karibu na watoto wao.Inasikitisha leo hii kuona watoto wakijiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, wizi, ulawiti, ngono na matukio mengine ambayo yanatokana na kukosa malezi bora.

Ni aibu mzazi au mlezi kulaumu walimu au dada wa kazi kutokana na tabia mbaya alizonazo mtoto. Mtoto anapoharibika, lawama si za mwingine ila mzazi wake.

Tunaamini ukaribu wa mzazi au mlezi ndiyo humfanya abaini kipaji alichonacho mtoto na kumuendeleza kulingana na mazingira na uwezo alionao.

Ukosefu wa malezi bora kuanzia katika ngazi ya familia umechangia Taifa kukosa watalaamu wazuri kwa kuwa vipaji vya watoto hukosa wa kuviendeleza huku wengine wakizuiwa kuvionyesha.

Vipaji tunavyoona kwa wachezaji wa mpira, wahandisi, walimu, madaktari, waandishi wa habari na taaluma nyingine, vingekuwa maradufu kama familia zingetenga muda mwingi kufuatilia makuzi na maendeleo ya watoto.

Mzazi au mlezi ana jukumu kubwa la kufuatilia maendeleo ya makuzi ya mtoto wake iwe shuleni au nyumbani, ili kujua tabia nzuri au mbaya alizonazo na kuweka mikakati ya kumnusuru au kumuendeleza.

Mzazi au mlezi kushtushwa na taarifa za mtoto wake kukamatwa kwa wizi, ulawiti, matumizi ya dawa za kulevya na matukio mengine maovu, ni ishara ya kutowajibika katika malezi.

Tunaamini mzazi au mlezi anapaswa awe wa kwanza kujua tabia nzuri au mbaya za mwanawe ili aweze kumtafutia msaada kwa wataalamu kama yeye atashindwa kumrekebisha au kumsaidia.

Tunawaomba wazazi na walezi wasione aibu kuomba ushauri au kuwafuata wataalamu wanapoona watoto wana tabia zisizofaa. Kunyamazia au kutetea uhalifu ni kuulea na baadaye utakuwa na madhara zaidi kwenye familia na hata jamii kwa ujumla.

Waswahili wanasema kinga ni bora kuliko tiba. Wazazi, walezi wasikwepe jukumu la ulezi wa watoto.