Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zahanati hii Mirerani ni mkombozi

Sehemu ya machimbo ya madini ya Tanzanite iliyopo Mirerani, Arusha. Picha na Mtandao

Katika mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kuna harakati za kiuchumi zinazosisimua Taifa.

Eneo hili ni kitovu cha madini ya kipekee duniani ya Tanzanite. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 12,000 huingia na kutoka kila siku katika kuta za machimbo haya, huku wengine 5,000 wakiwa ni wakazi wa kudumu ndani ya eneo hilo la uzalishaji.

Licha ya utajiri huu wa mabilioni ya shilingi, kwa miongo kadhaa eneo hili limekuwa "jangwa" la huduma za kijamii, hususan sekta ya afya.

 Kutokuwapo kwa hospitali, kituo cha afya, wala zahanati ndani ya ukuta wa migodi, imekuwa changamoto kubwa iliyogharimu afya na maisha ya wachimbaji wadogo.

 Hata hivyo, mwanga mpya umeanza kuchomoza kupitia uwekezaji wa kijamii unaofanywa na Kampuni ya Franone Mining.

Wataalamu wa haki za binadamu wanakubaliana kuwa haki ya kuishi ndiyo msingi wa haki nyingine zote.

Kwa miaka mingi, wachimbaji wa Mirerani wamekuwa wakipambana na maradhi kama malaria, homa ya matumbo, magonjwa ya mfumo wa upumuaji, na majeraha yatokanayo na milipuko ya baruti migodini bila kuwa na kimbilio la karibu.

Ujenzi wa zahanati mpya ndani ya ukuta wa Mirerani si tu jambo la kupongezwa, bali ni ukombozi wa kiutu.

Kitendo cha mchimbaji anayeugua kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika mji mdogo wa Mirerani kwenye vituo vya afya vya kata za Mirerani na Endiamtu, kilikuwa ni kero na hatari.

Uwepo wa zahanati hii sasa unakwenda kuziba pengo hili na kurejesha heshima ya mchimbaji mdogo.

Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandana, alifanya ziara ya ukaguzi na kujionea hatua kubwa iliyofikiwa katika ujenzi wa zahanati hiyo. Mradi huu ni tunda la maono ya uongozi mzima wa Kampuni ya Franone Mining.

Kwa kutumia zaidi ya Sh180 milioni, kampuni hii imeonyesha mfano wa kipekee wa kile kinachoitwa Uwajibikaji wa kampuni kwa Jamii ( CSR).

Zahanati hii itakayokabidhiwa kwa Serikali kwa ajili ya uendeshaji, itakuwa kimbilio la wachimbaji wasio na uwezo mkubwa wa kifedha, kwani huduma zitakuwa za gharama nafuu.

Hii ni hatua inayostahili kuigwa na wawekezaji wengine nchini, kuonyesha kuwa biashara si faida pekee, bali ni pamoja na kujali ustawi wa jamii inayozunguka mradi.

Zahanati hii haitaishia kwenye kutoa dawa na kutibu majeraha pekee. Itakuwa ni kituo cha kimkakati cha kuzuia magonjwa kazini.

 Eneo la Mirerani linasifika kwa vumbi la miamba ambalo husababisha magonjwa sugu ya mapafu na kifua kikuu. Kupitia zahanati hii, wataalamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Ambu (Kibong’oto) mkoani Kilimanjaro watapata kituo cha kufanyia kliniki za mara kwa mara.

Hii itasaidia katika upimaji wa mapema kwa kubaini wachimbaji walioathirika na vumbi na TB kabla hali zao hazijawa mbaya.

Pia wataalamu wa afya watatoa mafunzo ya uchimbaji salama, ikiwemo matumizi ya vifaa kinga na umuhimu wa kumwaga maji migodini ili kupunguza vumbi.

Jingine ni kutoa elimu ya afya ya akili na lishe kwa wachimbaji ambao mara nyingi hufanya kazi katika mazingira magumu na yenye msongo wa mawazo.

Ni vyema kutambua kuwa mradi wa zahanati hii ni mwendelezo tu wa rekodi ya Franone Mining katika kusaidia jamii. Kampuni imekuwa mstari wa mbele katika ukarabati wa miundombinu ya barabara zinazoelekea migodini, ujenzi wa vyumba vya madarasa na kusaidia shule za msingi na sekondari Simanjiro.

Pia uboreshaji wa mazingira ya kuhifadhia miili katika kituo cha afya Mirerani na kutoa misaada ya dharura kwa waathirika wa mafuriko katika Tarafa ya Moipo.

Mchango huu unajenga uhusiano mwema kati ya mwekezaji na jamii. Ni wito wangu kwa wakazi na wadau wa Mirerani kuwaunga mkono wawekezaji hawa.

 Migogoro isiyo na tija hurejesha nyuma maendeleo; badala yake, ushirikiano ndio utakaofanya miradi kama hii ya afya kuwa endelevu.

Tunapoipongeza Franone Mining, tunaisubiri kwa hamu siku ya uzinduzi wa zahanati hii.

 Ni matumaini yetu kuwa itakuwa kichocheo cha mabadiliko makubwa ya kidemografia na kijamii Mirerani, ambapo mchimbaji hatalazimika kupoteza maisha kwa kukosa huduma ya kwanza, na ambapo afya itathaminiwa sawa na thamani ya madini ya Tanzanite yenyewe. Afya ni uhai, na uhai ndio msingi wa uchumi wetu.