Serikali iongeze fedha bajeti ya afya

Muktasari:

Kiasi hicho hata hivyo ni pungufu kwa asilimia 19 ya bajeti inayomalizika ya mwaka 2017/18, ambayo wizara hiyo ilitengewa kiasi cha Sh1.07 trilioni.

Juzi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilisoma hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/19 na kuomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh898.3 bilioni.

Kiasi hicho hata hivyo ni pungufu kwa asilimia 19 ya bajeti inayomalizika ya mwaka 2017/18, ambayo wizara hiyo ilitengewa kiasi cha Sh1.07 trilioni.

Tukiwa sehemu muhimu ya wadau wa afya na maendeleo ya nchi kwa jumla, tunalazimika kuhoji sababu za bajeti hiyo kupunguzwa, hasa katika kipindi hiki ambacho sekta ya afya inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Sekta ya afya kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto tete kama vile uhaba wa vifaa tiba, dawa, watumishi wasiotosheleza mahitaji na nyinginezo nyingi ambazo ili kuzitafutia ufumbuzi, wizara inahitaji kuwa na fungu la kutosha la bajeti.

Katika mazingira ambayo wadau wengi wangetarajia kuona sekta ya afya ikiongezewa bajeti kuzidi hata ile ya mwaka 2017/18, inasikitisha kuwa Serikali haijaona umuhimu wa kuinusuru sekta hii nyeti kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa jumla.

Mshangao zaidi unatupata kwa kuwa nchi yetu ni kati ya nchi zilizosaini Azimio la Abuja mwaka 2001 linalozitaka bajeti za nchi kutenga asilimia 15 ya bajeti zao kwa ajili ya sekta ya afya.

Ikiwa tungetekeleza azimio hili, bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2018/19 ingekuwa Sh4.84 trilioni, kiasi ambacho sisi tuna imani kubwa kuwa kingeweza kufanya makubwa katika sekta ya afya.

Afya ni sekta mtambuka. Ni sekta inayogusa sio tu ustawi wa wananchi, lakini hata nyanja nyingine za kijamii na kiuchumi, hivyo kuipunguzia bajeti ni sawa na kuchochea moto wa kudorora kwa sekta nyingine zinazotegemea uimara wa sekta mama ya afya.

Kwetu sisi, upungufu huo wa fedha sio tu una madhara mengi ikiwamo kusababisha athari kubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi, lakini pia unaweka rehani utekelezaji wa vipaumbele 12 vya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 na hata kufifisha Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya- IV.

Sekta ya afya inahitaji mipango, mikakati na utekelezaji thabiti. Vyote hivi haviwezi kufanikiwa bila ya kuwapo kwa rasilimali fedha kama nyenzo kuu ya kuchochea maendeleo ya sekta.

Kama Taifa tunahitaji kuwa makini kwa kuchagua sekta ya afya kuwa moja ya vipaumbele muhimu vya kibajeti.

Tanzania mpya ya viwanda na yenye dhamira ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2015 inahitaji pamoja na mambo mengine nguvu kazi ya watu wenye afya bora.

Ubora huu wa afya kwa wananchi hauwezi kufikiwa kwa kupunguza uwekezaji kwenye sekta ya afya. Tunaitazama hatua hiyo kama ishara ya kufifisha dhamira na jitihada za kuiendeleza nchi yetu.

Ikiwa sekta hii nyeti haitapewa kipaumbele katika mipango ya nchi hasa upande wa bajeti, tukubali kuwa itakuwa ni ndoto kuifikia Tanzania ya viwanda iliyo imara na madhubuti.