Zamani muziki ilikuwa lazima ujue kuandaa melodi ya wimbo wako

Muktasari:

Nilipokuwa nausikiliza wimbo wake nimependa sana uimbaji wake lakini nilikuwa na shida kuelewa mpangilio wa vyombo katika muziki huo, hivyo nilitaka kujua aina ya vyombo alivyotumia na pia alikuwa ana sababu gani kutumia vyombo hivyo.

Juzi nilikuwa naongea na msanii maarufu ambaye ana wimbo ambao siku hizi haukosi kupigwa hewani mara tatu kwa siku. Kizazi chake wanasema “ametoka”. Nilikuwa na maswali machache kwa supastaa huyu.

Nilipokuwa nausikiliza wimbo wake nimependa sana uimbaji wake lakini nilikuwa na shida kuelewa mpangilio wa vyombo katika muziki huo, hivyo nilitaka kujua aina ya vyombo alivyotumia na pia alikuwa ana sababu gani kutumia vyombo hivyo.

Kifupi tu alishangaa swali hilo na alikuwa hana jibu. Alisema aliyepanga hivyo vyombo si yeye bali mtayarishaji wake. Jibu lake lilinirudisha nyuma sana wakati nikiwa katika bendi miaka ya 1980 jinsi tulivyokuwa tukitunga na hatimaye kurekodi nyimbo.

Katika zama hizi msanii hutunga ‘mistari’ yake na kufanya mazoezi ya kuuimba peke yake kisha huingia studio ambako mtayarishaji humtengenezea muziki au maarufu ‘beat’.kutoka hapo wimbo huenda hewani.

Hali ilikuwa tofauti huko nyuma. Labda nirudishe picha miaka ya 1980 mwishoni nilipokuwa Bendi ya Tancut Almasi iliyokuwa na maskani yake Iringa.

Mwanamuziki yeyote mwenye uwezo wa kutunga aliruhusiwa kutunga wimbo, watunzi walikuwa wa aina tofauti. Watunzi maarufu mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa walikuwa wakitunga pamoja, hivyo walikuwa wakileta wimbo ambao umekwishapangwa sauti za uimbaji na hata magitaa ya kusindikiza ambayo waliyaimba kwa mdomo.

Lakini watunzi wengine walikuja na mashairi na kutegemea watu wengine watunge sauti na kupanga vyombo. Lakini kitu cha kwanza ambacho kilikuwa kinafanyika kwa tungo yoyote ile ilikuwa ni mtunzi kuyasoma mashairi yake mbele ya watu wote.

Baada ya hapo ndipo mtunzi alianza kuuimba wimbo huo wakati waimbaji wenzake wakimsikiliza na kuchangia hapa na pale kuuboresha. Baada ya hapo waimbaji walianza kupangiana sauti ili kuleta muafaka katika wimbo huo.

Wakati huo mpiga gitaa mmoja mara nyingi gitaa la rhythm alikuwa akisindikizana na waimbaji wakati wa kuanza kujenga njia za wimbo huo. Baada ya hapo wapiga magitaa wote walikaa pembeni na kupanga magitaa yao.

Vyombo vya upulizaji vilifuata na hatimaye wimbo ulikuwa tayari. Bendi iliufanyia mazoezi kati ya wiki moja au mbili kabla ya kuanza kuupiga hadharani.

Siku ambayo wimbo ulikuwa unapigwa kwa mara ya kwanza hadharani kila mwanamuziki wakiwemo mafundi mitambo hata marafiki wa karibu wa bendi walikuwa wakiangalia wimbo umepokewa vipi na wapenzi.

Wimbo ukionekana umepigwa mara mbili au tatu lakini haujapokewa vizuri, ulirudishwa tena mazoezini au mara nyingine ulikufa hapohapo na haukupigwa tena, labda mtunzi angeupika tena.

Wimbo ukipata bahati ya kurudi mazoezini watu waliulizana kwa nini haukupokewa vizuri, na kwa kweli watu walikuwa wanapeana ukweli kiasi cha kwamba mara nyingi baada ya kufanyiwa marekebisho wimbo uliweza kupokewa vizuri na kuingizwa katika orodha ya nyimbo za kurekodiwa.

Nyimbo zilipigwa ukumbini kwa muda wa miezi kadhaa kabla ya kurekodiwa, hivyo ‘kuuivisha’ kwa maboresho ya hapa na pale kila ulipopigwa ukumbini.

Bendi zilikuwa zikirekodi nyimbo zao katika studio za RTD. Taratibu zilizokuwepo ni kuwa kabla ya kupangiwa siku ya kuingia studio, bendi zililazimika kupeleka RTD mashairi ya nyimbo zote ambazo zinatakiwa kurekodiwa.

Huko kulikuwa na kamati ambayo iliyapitia mashairi hayo na kuidhinisha kurekodiwa au kukataa kurekodiwa nyimbo ambazo zilionyesha kuwa na tungo tata.

Nyimbo nyingi zilipita bila kupingwa kwa kuwa bendi zilikuwa zinafanya kikao cha ndani cha kuangalia upya mashairi kabla ya kuyapeleka RTD. Lakini pamoja na matayarisho hayo, bado nyimbo kadhaa zilikwama au nyingine kukatazwa kurushwa hewani japo zilikuwa zimepita katika kamati ya awali.

Siku hizi mtu anaweza kuchukua mwezi mzima kurekodi wimbo mmoja. Hali haikuwa hivyo zamani, RTD walikuwa wakitoa siku mbili kwa kila bendi kuwa studio.

Siku ya kwanza kurekodi nyimbo zote, hata kama ni 15. Na muda wa mwisho kuwa studio ilikuwa ni saa 12 jioni, hivyo ilikuwa muhimu kufanya sana mazoezi kabla ya kuingia studio ili kutumia vyema muda huo. Siku ya pili bendi ilishiriki katika kurekodi kipindi cha Klabu Raha Leo Show.

Ni wazi ukielewa aina ya ugumu wa taratibu za kurekodi na kuona kuwa nyimbo zilizorekodiwa katika mazingira hayo bado ni maarufu miaka hamsini baada ya kurekodiwa, mtu unaelewa ubora wa wanamuziki katika miaka hiyo.

Kutokana na aina ya kurekodi mwanamuziki ulijua kabisa ni vyombo gani vimetumiwa katika wimbo wako na kwa nini chombo fulani kimepigwa katika sehemu fulani. Hakika kila zama na vitabu vyake.