Anna Mghwira, mwanamke pekee aliyejitosa kuwania urais

Mgombea urais kupitia kupitia tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira akikabidhiwa nyaraka za uchaguzi Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Damiani Lubuva. PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Elimu yake na ujasiri vinampa sifa ya kusimama katika nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.

Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama kipya cha siasa, ACT – Wazalendo.Alizaliwa Januari 23, 1959 katika hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao Manispaa ya Singida Mjini.

Baba mzazi wa Anna alikuwa diwani na kiongozi wa Tanu kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walipata watoto tisa, akiwamo Anna.

Mghwira alianza safari ya kielimu katika Shule ya Msingi Nyerere Road mwaka 1968 – 1974 akaendelea na sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978, kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya sekondari katika Seminari ya Lutheran kati ya mwaka 1979 – 1981.

Aliendelea na masomo ya chuo kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Theolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu Shahada ya Theolojia mwaka 1986. Mwaka huohuo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria.

Kati ya mwaka 1987 na 1998, Anna aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa. Safari ya elimu ya Mghwira ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza ambako alianza Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa shahada hiyo mwaka 2000.

Licha ya kuwa mwanasheria na mwanatheolojia aliyebobea, Anna amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa, utumishi katika mashirika ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.

Anna ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.

 

Safari yake kisiasa

Alianza siasa tangu wakati wa Tanu akiwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika Tanu lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.

Kwa kipindi kirefu, hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za uenyekiti wa baraza la wanawake ngazi ya wilaya na katibu wa baraza la wanawake mkoa. Machi mwaka huu alijiunga rasmi na ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa ACT.

Aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mumewe hivi sasa ni marehemu.

 

Mbio za ubunge

Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.

Alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa. Hata hivyo, chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari (Joshua) na Mghwira alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho. Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.

 

Urais AC T-Wazalendo

Jambo la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni umahiri wake katika elimu. Yeye ni msomi nguli wa masuala ya sheria lakini ana shahada tatu za vyuo vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa nyingine, iongozwe na Rais ambaye elimu si kikwazo kwake.

Kwa nchi kama Tanzania ambayo mfumo dume umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu, Anna anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa.

Kwa sababu Anna ni mwanamke imara na anayepambana kwa muda mrefu sasa. Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni baraka tosha kwa siasa za kisasa ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali na kutafuta mchango wa wanawake katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jinsia yake inampa fursa ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika jamii ambayo inazidi kupoteza imani na uaminifu wa wanaume.

Anna pia ana uthubutu. Alipambana na changamoto za ndoa na shule. Wanawake wengi huchagua kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye alikwenda nayo yote na kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu vinamfanya kuwa mwanamama imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi kubwa.

Pamoja na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha wa kukaa nje ya nchi na kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa, Anna ni mwanamama wa kawaida sana.

Watu wa karibu naye wanamtaja hivyo. Si mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda kuandika makala za kuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea na kujichanganya na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada. Sifa zote hizi ni nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji uongozi mkubwa wa nchi.