Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ni awamu ya kazi, tuchape kazi

Rais Magufuli akikagua gwaride

Muktasari:

Akitambua kuwa uvivu ni chukizo na Serikali yake haitakuwa na nafasi ya watu wanaoishi kama kunguni, kula vitu vya bure, kutojali kazi, Dk Magufuli aliweka msisitizo wa wazi tena mapema kwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu.

Katika kipindi chote cha kampeni za kuwania urais, Dk John Magufuli amekuwa akiwataka wananchi kujipanga kufanya kazi kwa sababu Serikali yake haitavumilia watu wavivu. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu “mvivu” ni mtu asiyependa kufanya kazi; mtepetevu, mkunguni; mlegevu, mzembe.

Akitambua kuwa uvivu ni chukizo na Serikali yake haitakuwa na nafasi ya watu wanaoishi kama kunguni, kula vitu vya bure, kutojali kazi, Dk Magufuli aliweka msisitizo wa wazi tena mapema kwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu.

Kaulimbiu hiyo yenye maana kubwa kiutendaji ni mwendelezo wa kaulimbiu za awamu mbili zilizopita. Serikali ya Awamu ya Tatu iliingia na kaulimbiu ya Ukweli na Uwazi msisitizo ukiwa kwa watendaji kufanya kazi kwa uwazi na kuwa wakweli ndiyo maana ilianzisha idara ya wasemaji wa kila wizara.

Kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa kurejesha ari, nguvu na kasi katika utendaji kazi ndiyo maana ilijipambanua kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya na baadaye Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi.

Baada ya kuwapo uwazi na ukweli katika utendaji na utoaji habari, na kurejeshwa ari, nguvu na kasi katika utendaji, Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ili kuhimiza watendaji serikalini, na wananchi kuchapa kazi.

Ujumbe wake ulikuwa wazi. Katika maeneo mengine wakati wa kampeni alikuwa akisisitiza; “Tujipange kufanya kazi, hata maandiko ya vitabu vitakatifu yanasema, asiyefanya kazi asile…”

Hata alipoapishwa rasmi juzi kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano, Dk Magufuli alisisitiza “sasa kazi tu” ikiwa na maana kaulimbiu hiyo haikuwa ya kufurahisha wapigakura bali dhamira ya kweli kutaka kuleta mabadiliko ya kweli kiutendaji serikalini na maeneo ya uzalishaji viwandani na mashambani.

Tena hakumung’unya maneno. Mahali pengine alionya kuwa wazembe, wavivu na wapigadili maofisini waanze kufungasha virago. Hivyo, tunaamini amechagua kaulimbiu hiyo akilenga mabadiliko ya kweli kwamba wafanyakazi waache uzembe na wananchi waache uvivu; vijana waache utegemezi ili kila mtu afanye kazi.

Mabadiliko ya kweli lazima yamhusu kila mwananchi anayetaka maisha bora maana wajibu wa Serikali ni kutengeneza fursa siyo kugawa fedha, nyumba, mavazi na vitu; wanaotaka kuondoa nyumba za tembe lazima wafanye kazi, na wanaotaka kuondokana na umaskini lazima waonyeshe juhudi za kuukataa umaskini kwa kufanya kazi.

Mvunjanchi ni mwananchi na atakayeleta maendeleo ni mwananchi. Kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu, inahimiza na kuchochea utiifu, uaminifu, uzalendo; kuzuia wezi na waharibifu wa mali ya umma, kudhibiti ufisadi na uzembe ili kujieletea maendeleo.

Hii ni kaulimbiu inayomsukuma kila mwananchi kutimiza wajibu wake kuanzia maofisini, viwandani hadi mashambani ili ale kwa jasho lake. Wafanyakazi wengi huchelewa sana kuingia kazini lakini wanakuwa wa kwanza kuondoka kurudi majumbani kwao bila kujali wamesababisha hasara au wametoa mchango wenye tija.

Vilevile, tunaamini kwamba kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu itawachochea watendaji wa ngazi mbalimbali serikalini kuanzia mawaziri hadi wa chini kutimiza wajibu wao ipasavyo bila kusukumwa wala kusimamiwa.

Hali tukiunga mkono kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu tunawasihi wananchi wachukie uvivu, uzembe na waache kulalamikia ovyo viongozi wao hata kwa mambo yaliyo chini ya uwezo wao.