MAKALA: Dk Ndalichako ni mtu sahihi Wizara ya Elimu
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dk Joyce Ndalichako
Muktasari:
Nakumbuka katika ripoti ya kwanza ya utekelezaji wa BRN kwa mwaka 2013/14, iliyotolewa Machi mwaka huu ilionyesha mafaniko katika sekta zote sita zilizopo katika mpango huo, hakuna iliyopata chini ya asilimia 50.
Mipango mingi imepangwa, ukiwamo ule wa Matokeo Makubwa sasa (BRN) lengo likiwa ni kuhakikisha nchi inapata mafanikio katika sekta mbalimbali.
Nakumbuka katika ripoti ya kwanza ya utekelezaji wa BRN kwa mwaka 2013/14, iliyotolewa Machi mwaka huu ilionyesha mafaniko katika sekta zote sita zilizopo katika mpango huo, hakuna iliyopata chini ya asilimia 50.
Sekta ya elimu ilipata asilimia 81, Maji asilimia 80, Nishati asilimia 79, Kilimo asilimia 77, Uchukuzi asilimia 64 na Utafutaji wa Rasilimali asilimia 54.
Wengi walipingana na ripoti hiyo, hasa kuitaja elimu kuwa kinara kutokana na shule nyingi nchini kutokuwa na miundombinu muhimu inayohitajika, walimu kuendelea kuidai Serikali, huku kukiwa na kasoro lukuki katika sera ya elimu licha ya kuandaliwa kwa miaka saba.
Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli kumteua Dk Joyce Ndalichako kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Hakika ni mtu sahihi.
Mwaka 2013 Dk Ndalichako akiwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), alijiuzulu baada ya asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2012 kupata alama sifuri na kukawapo na shinikizo la kisiasa la kutaka kubadili matokeo hayo lakini alikataa.
Katika miaka ya hivi karibuni taifa limeshuhudia anguko kubwa la kiwango cha ubora wa elimu nchini licha ya juhudi za Serikali kuboresha sekta ya elimu kupitia mipango mbalimbali.
Mijadala kuhusu elimu yetu na mustakabali wa maendeleo ya Taifa kwa miaka ijayo, ni mjadala unaokuja kama matokeo ya changamoto zinazoendelea kuikabili sekta ya elimu.
Elimu ni mchakato unaowezesha mtu kupata maarifa na ujuzi wa kujitambua na kujiweka sawa katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika mazingira na mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia.
Elimu ni nyenzo ya kumwezesha mtu kutambua uwezo na wajibu wake kamili katika jamii, madhumuni ya elimu Tanzania ni kuongoza na kukuza maendeleo ya utu wa Watanzania, ujuzi wao na kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo, ili kuleta maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla.
Kama tunahitaji kusonga mbele kama Taifa lazima tuwe na mfumo bora wa elimu. Nasema hivi kwa sababu mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu kwa miaka ijayo, unajengeka katika upatikanaji wa elimu bora kwa watu wote, jambo ambalo ndio kiini cha kufanikisha kufikiwa kwa madhumuni mapya ya elimu.
Ili tusonge mbele ni lazima kuibua uwezo wa Mtanzania kufikia kiwango cha juu kwa kumwezesha aendelee kujifunza katika maisha yake yote, kuishi katika dunia iliyo salama na yenye mafanikio kwa wote.
Nini kifanyike ili kuinua elimu yetu? Kuna masuala mengi kwa upana wake katika hoja hii yakiwamo ya kuinua mafunzo ya ualimu, mitalaa, lugha ya kufundishia, usimamizi bora wa elimu na wajibu wa wadau wa elimu katika kujenga msingi wa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Haya ni masuala machache ambayo tunategemea juhudi za Serikali. Ila kumbuka kuwa mambo hayo hayawezi kutimia kama tutakuwa na waziri wa elimu mzigo.
Dk Ndalichako ni mkereketwa wa elimu na amekuwa katika taaluma hiyo kwa muda mrefu. Ni Waziri ambaye akikwambia atatatua kero za elimu hutakuwa na shaka kuamini maneno yake.
Msimamo wake ndio uliomng’oa Necta, sasa amepewa rungu ambalo naamini kwa ubora wake ataweza kulitumia kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu.
Lakini pamoja na uteuzi wake, sasa Serikali ya Awamu ya Tano inapaswa kuweka mfumo imara wa utendaji wa kazi na si mawaziri kuendelea na matamko kama tunayoyaona sasa. Matamko haya hayana tija. Nchi haiwezi kuendeshwa kwa matamko kwa miaka mitano.
Lazima changamoto, kero na uozo nilioutaja hapo juu uundiwe mikakati ya kuumaliza. Historia nzuri ya utendaji kazi wa waziri unaweza kufichwa na mfumo mbovu.
Mfano ni uteuzi wa Dk Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Waziri huyo alifanya makubwa katika ukusanyaji wa mapato ndani ya muda mfupi aliokuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Uchapakazi wa Dk Mpango kila mtu anaujua lakini ataweza kwa mfumo huu tulionao? Vipi kuhusu Waziri wa Maliasili na Utalii kwa Profesa Jumanne Maghembe.
Profesa Maghembe aliwahi kuitwa mmoja wa mawaziri mizigo na chama chake CCM kikimtaka Rais mstaafu Jakaya Kikwete amtimue. Leo kapewa wizara je ule ‘mzigo’ ameutua. Mawaziri wa namna hii ambao walionekana mizigo ndani ya vyama vyao wataziweza wizara walizopewa chini ya mfumo huu tulionao sasa? Tusubiri muda utazungumza.
Nampongeza Dk Ndalichako ila nilishangazwa na Profesa Makame Mbarawa kuhamishwa wizara ndani ya wiki mbili tu tangu alipoteuliwa. Sijui kilichotokea ila kama nilivyosema awali muda utazungumza acha tusubiri.
0754 597315