MAONI : Mkataba wa Simba, Singano tuambiwe ukweli

Ramadhan Singano ' Messi'

Muktasari:

Michezo katika nchi yetu ilikuwa ya ridhaa, kiasi cha wengi kucheza kwa mapenzi au wakati mwingine kujiburudisha, ingawa siku hizi imebadilika na kuwa ajira kwa vijana, wakiwamo wanasoka ambao wameajiriwa na wanaishi kwa kutegemea michezo.

Tanzania, siku zote imekuwa ni nchi inayoendeshwa kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zinazosimamia sekta mbalimbali, ikiwamo michezo ambako kwa siku za karibuni imeshuhudia mabadiliko makubwa.

Michezo katika nchi yetu ilikuwa ya ridhaa, kiasi cha wengi kucheza kwa mapenzi au wakati mwingine kujiburudisha, ingawa siku hizi imebadilika na kuwa ajira kwa vijana, wakiwamo wanasoka ambao wameajiriwa na wanaishi kwa kutegemea michezo.

Katika michezo, licha ya nchi yetu kutofanya vizuri kitaifa na kimataifa kwa miaka mingi, siku hizi kumeibuka matukio ambayo yakiachwa yaendelee kama yalivyo, ipo siku yataiharibu sifa au taswira nzuri ya michezo kuwa ajira, burudani na wakati mwingine biashara.

Ipo mifano ya matukio ambayo yamejitokeza katika michezo katika siku za karibuni ambayo yakiachwa, nchi yetu itazidi kupoteza mwelekeo.

Kubadilika kwa mfumo wa uendeshaji wa michezo kumewafanya baadhi ya wanamichezo kuingia mikataba na klabu wanazozitumikia kwa mwaka au zaidi.

Mfano ni mgogoro wa kimkataba baina ya mshambuliaji wa Simba, Ramadhan Singano ‘Messi’ na klabu hiyo ambao umekuwa ukiendelea kwa muda huku kila upande ukilaumu mwingine kwa madai ya kuukiuka.

Mgogoro huo, kwa sasa umechukua sura mpya inayozidisha utata baada ya juzi, Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuamua kuwa mchezaji huyo ni huru, hana mkataba na Simba inayodaiwa kukiuka vipengele vya kimkataba, kikiwamo cha kumpatia mahali pa kuishi.

Tunasema, uamuzi wa kamati hiyo umezidisha utata ulioanzia TFF ilipoamuru Singano na Simba wakae mezani kujadili mkataba ambao klabu hiyo ilidai inao na mchezaji huyo hadi mwaka 2016, wakati Singano akidai mkataba wake unaishia mwaka huu.

Kwa bahati mbaya, TFF ambayo ndiyo mtunzaji wa mikataba ya wachezaji wa klabu zao ni kama ilikuwa inajaribu kufunika kombe mwanaharamu apite, kwa kutaka klabu hiyo (Simba) ikae na Singano na kujadili mkataba ambao hatuambiwi ni nani aliyeukiuka.

Kwa sababu hiyo, tunaitaka TFF itoke hadharani ieleze wadau wa michezo na Watanzania ni nani kati ya Singano na Simba aliyekiuka au kughushi mkataba ambao pande hizo mbili zimekuwa zikidai kuwa nao, kiasi cha kuambiwa zikae na kujadiliana.

Kwa kushindwa kufanya hivyo, TFF itakuwa inaficha kitu au pengine inaogopa kuumbuka, ingawa kwa uamuzi huu uliotolewa juzi na kamati yake ikieleza kuwa mchezaji huyo ni huru, ni sawa na kutotambua uamuzi wa awali wa TFF kuzitaka pande hizo zikutane na kujadiliana.

Tunaamini, suala hili la kubadilishwa kwa vipengele vya mkataba baina ya Singano na Simba, lina kila dalili ya kuwapo kwa upande ulioghushi mkataba au makubaliano, jambo ambalo ni kosa la jinai. Tunaamini, kughushi mkataba au makubaliano yoyote ni kosa la jinai ambalo TFF kama mtunzaji wa kumbukumbu, ikiwamo mikataba ya wachezaji, lazima iwajibike kueleza kilichotokea, ni nani hasa aliyeghushi mkataba huo.

Kama TFF haitaki kusema ukweli, tunaamini vipo vyombo vingine vya umma au dola kama Polisi, yenye wataalamu wa uchunguzi wa masuala hayo ya makosa ya jinai, kwa nini wasitumike kufanya uchunguzi wa kina na kubaini ni nani baina ya Singano na Simba aliyeghushi mkataba ili achukuliwe hatua za kisheria ili liwe fundisho kwa wengine?