Ni maendeleo au kifo cha taarab?
Muktasari:
Hapo mwanzo alikuwapo Sitti binti Saad, mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kurekodi muziki wake kwenye albamu; alikuwa akiimba taarab, muziki wenye asili ya Misri uliongia visiwani Zanzibar kwa udhamini wa Sultan wa Pili wa visiwa hivyo, Bargash bin Said.
Hapo mwanzo alikuwapo Sitti binti Saad, mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kurekodi muziki wake kwenye albamu; alikuwa akiimba taarab, muziki wenye asili ya Misri uliongia visiwani Zanzibar kwa udhamini wa Sultan wa Pili wa visiwa hivyo, Bargash bin Said.
Kisha akaja Malkia wa taarab na muziki wa Unyago, Fatuma binti Baraka maarufu kama Bi kidude, ambaye aliwahi kukiri kwa kinywa chake kwamba alijifunza kuimba taarab kutoka kwa Sitti binti Saad.
Bi Kidude na mwalimu wake Sitti wameshatangulia mbele za haki, lakini muziki waliokuwa wakiufannya bado upo na unaishi. Zipo bendi na hata wanamuziki binafsi wanaendelea kuimba taarab ingawa si kama taarab iliyokuwa ikifanywa na wakongwe hao.
Hiko ni kitu cha kawaida, muziki una tabia ya kubadilika kadri ya muda unavyokwenda. Hasa hubadilika mapigo, aina za melodi, uandishi wa mashairi na kadhalika lakini maadhi hubaki palepale; yaani hata kama wimbo ulitengenezwa miaka 800 iliyopita ukiusikia tu utagundua kuwa hii ni Hip Hop, hii ni Ragga na ndiyo maana leo hii kuna ‘morden taarab’ na ‘taarab asilia’.
Lakini mabadiliko ya taarab yanashangaza zaidi ya kawaida, unashindwa kuelewa kama aina hiyo ya muziki imebadilika au ilishakufa na haipo tena duniani.
Kuna baadhi ya nyimbo ukizisikiliza husikii ‘utaarab’ wowote ndani yake lakini wenye nyimbo zao huzitambulisha kuwa ni taarab na mashabiki wanalazimika kuzipokea hivyo na kuziomba kwenye vipindi maalum vya muziki wa taarab.
Wapo walioamua kujipa uhuru na kuunda aina mpya ya muziki wanayoiita ‘Taradansi’;yaani ni muziki uliotokana na mchanganyiko wa taarab na muziki wa dansi.
Hawa wako sahihi kwa sababu si dhambi kuunda aina mpya ya muziki kwani hata taarab yenyewe ni mchanganyiko wa muziki kutoka nchi zenye mila na desturi za kiarabu na Afrika. Lakini dhambi kubwa inayokera na kuchefua ni kuwadanganya mashabiki; kufanya nyimbo ya dansi na kuibatiza utaarab kwa lazima.
Huko ni kuiua taarab, kwa sababu mambo yatakwenda hivyo na vizazi vipya vitakuja kuishi na taarab ambayo haina utaarab wa aina yoyote ndani yake.
Kwa sababu si wengi watakaokuwa wakifahamu chimbuko la muziki huo, wataitukuza taarab bandia na kuirithisha kwa vizazi na vizazi.
Taarab ni moja ya tunu za sanaa tulizojaliwia Watanzania, ni muziki ambao unaweza kutumika kama kielelezo kizuri cha taifa hili; ni kama ambavyo muziki wa Kwaito unavyoitambulisha vema Afrika kusini, taarab inaweza kutumika namna hiyo kwa sababu kwanza historia imeweka wazi kwamba muziki huo uliingia afrika kupitia Tanzania visiwani.
Lakini pia, hadi leo taarab inaimbwa na kuchezwa sana Tanzania zaidi ya nchi yoyote ile duniani, hiyo ni kwa sababu wakongwe waliokuwepo walijitahidi kuitangaza sana na kuienzi vilivyo.
Umefika wakati kwa wasanii wa taarab muwe wa wazi kwa mashabiki, kama umefanya wimbo ambao si taarab basi waeleze ukweli kuliko kudanganya kwani katika muziki si vibaya kwa msanii kufanya vitu nje ya ulivyozoeleka na mashabiki. Unaruhusiwa kufanya taarab na hata dansi kama unamudu na ipo mifano ya wazi ya waimba taarab wanaofanya muziki wa dansi na hata bongofleva pia, lakini hawachanganyi mambo, hawathubutu A kuifanya BA
Pia vyombo vyetu vya habari vinavyofanya kazi za kupokea na kutangaza nyimbo hizi ni vyema vikawa na vitengo maalum vya uchambuzi wa nyimbo zote zinazopokelewa na sio jukumu la kutaja maadhi ya nyimbo lifanywe na msanii mwenyewe wakati wakuitambulisha hasa ukizingatia tuna wasanii wengine wasioulewa muziki vizuri kiasi cha kushindwa hata kufafanua aina ya muziki wanaoufanya.
Taarab ni tunu, tuilinde, tuithamini.
0713 482 816