Rais Obama kaondoka, tusirudie maisha ya aibu

Rais Obama na mkewe wakiwaaga mamia ya wananchi na viongozi waliojitokeza kumuaga katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Muktasari:

Kama tulivyosema jana katika safu hii, ziara hiyo sio tu ilikuwa ya mafanikio makubwa, bali pia ilikuwa ya kihistoria na tunadiriki kusema hapa kwamba kumbukumbu ya ziara hiyo haitaweza kufutika kirahisi katika mioyo ya Watanzania katika miaka mingi ijayo.

Ziara ya siku mbili ya Rais wa Marekani, Barack Obama hapa nchini ilimalizika juzi mchana ambapo kiongozi huyo na familia yake waliwaaga Watanzania na kurejea makwao.

Kama tulivyosema jana katika safu hii, ziara hiyo sio tu ilikuwa ya mafanikio makubwa, bali pia ilikuwa ya kihistoria na tunadiriki kusema hapa kwamba kumbukumbu ya ziara hiyo haitaweza kufutika kirahisi katika mioyo ya Watanzania katika miaka mingi ijayo.

Sio nia yetu kuorodhesha tena hapa mafanikio yaliyotokana na ziara ya kiongozi huyo. Pamoja na kwamba tulifanya hivyo katika tahariri ya toleo la gazeti hili jana, vyombo vingi vya habari nchi nzima pia viliandika na kuitangaza ziara hiyo kwa kiwango cha juu. Uzoefu wetu umeonyesha kwamba ni nadra sana kwa vyombo vya habari kuwa na mtazamo mmoja katika suala kubwa kama hili. Lakini jambo la kutia moyo ni kuwa, vyombo vya habari vinakubaliana kwamba ziara hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa na kwamba taifa letu litafaidika sana kiuchumi.

Tunawapongeza wote walioshiriki kufanikisha ziara hiyo. Kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete jana, ziara hiyo isingefanikiwa kiasi hicho pasipo umoja, ushirikiano, uzalendo na mshikamano ulioonyeshwa na wananchi, vyombo vya habari, vyombo vya dola na taasisi mbalimbali za kiserikali na kiraia. Tunakubaliana na Rais Kikwete kwamba mafanikio ya ziara hiyo kwa kiasi kikubwa yametokana na ukweli kwamba Rais Obama aliwakuta Watanzania wakiwa kitu kimoja ndani ya nyumba moja na ndio maana kwa ujumla wao waliupokea ugeni huo kwa bashasha na hamasa kubwa.

Vyombo vya habari vya Marekani na kwingineko duniani vilitangaza kwamba Rais Obama alipata mapokezi ya kihistoria nchini Tanzania tofauti sana na aliyopata katika nchi za Senegal na Afrika ya Kusini alikoanzia ziara yake hiyo ya siku saba katika nchi tatu barani Afrika. Jambo hilo la ukarimu kwa wageni ni moja ya tunu tulizopewa na Mwenyezi Mungu na pia ni moja ya mambo yanayoipambanua na kuitofautisha nchi yetu na nchi nyingine nyingi.

Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa, kwani hakuna mhisani au mwekezaji mwenye akili timamu atakayetamani kutoa misaada au kuwekeza katika nchi ambayo watu wake wanagombana na kutoana macho. Hivyohivyo, hakuna mwekezaji mwenye sifa za kuitwa mwekezaji atakayependa kuweka mitaji yake katika mazingira yatakayohatarisha mitaji hiyo. Hivyo, ni dhahiri kwamba wafanyabiashara wakubwa waliofuatana na Rais Obama waliridhika na mazingira tuliyo nayo kwa uwekezaji na Rais huyo aliwaambia pasipo kutafuna maneno kwamba Tanzania ina mazingira maridhawa kwa kuwekeza na kufanya biashara.

Hoja ya msingi hapa ni kwamba huu hakika ni wakati wa kutumia fursa ya ziara ya Rais Obama nchini mwetu kujenga uchumi. Mazingira tuliyomtayarishia Rais Obama na ujumbe wake lazima tuyaendeleze, ikiwa ni pamoja na kutunza usafi wa mazingira, barabara, kuzoa takataka mitaani na kuhakikisha biashara zinafanyika katika sehemu zilizotengwa kwa ajili hiyo.

Ni kweli Rais Obama ameondoka. Hata hivyo, tusikubali kurudia maisha ya aibu ya kuishi katika mazingira machafu yanayoudhalilisha ubinadamu. Ziara hiyo imedhihirisha kwamba tunao uwezo kama taifa wa kuweka mazingira yetu katika hali ya usafi. Sasa mpira uko mikononi mwa viongozi waliopewa dhima ya kuongoza nchi, ikiwa ni pamoja na kusimamia usafi.