Tanzania haina sababu za kuiogopa ICC
Muktasari:
- Hivyo, lilikuwa jambo la kustaajabisha kuona viongozi wa nchi wanachama wa AU wakipiga kura Mei mwaka huu mjini Addis Ababa eti kurejesha kesi za Rais wa Kenya na Naibu wake nchini Kenya ili ziamuriwe na Mahakama za Kenya au za nchi jirani ya Tanzania.
Wakuu wa nchi za Afrika wanatarajia mwezi ujao kufanya kikao maalumu nchini Ethiopia kujadili juu ya kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Mkutano huo unafuatia ombi la Kenya kwa AU la kufanyika mkutano wa dharura kujadili kesi zinazowakabili Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto katika Mahakama hiyo iliyopo The Hague, Uholanzi.
Ikumbukwe kwamba viongozi hao wawili wanakabiliwa na mashtaka katika Mahakama hiyo, kutokana na ghasia zilizoikumba Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya 1,000 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 600,000 waliachwa bila makazi. Juhudi za wasuluhishi wa UN walioongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Kofi Annan hazikufanikiwa kwa kiwango kilichotarajiwa, kwani mbali na kuwasuluhisha mahasimu wakuu katika mgogoro huo na kuwawezesha kuunda Serikali ya Mseto, mahasimu hao walishindwa kuafikiana kuhusu kuundwa kwa Mahakama nchini Kenya ya kusikiliza kesi za uhalifu dhidi ya binadamu.
Hivyo, lilikuwa jambo la kustaajabisha kuona viongozi wa nchi wanachama wa AU wakipiga kura Mei mwaka huu mjini Addis Ababa eti kurejesha kesi za Rais wa Kenya na Naibu wake nchini Kenya ili ziamuriwe na Mahakama za Kenya au za nchi jirani ya Tanzania. AU kwa makusudi imekuwa ikipotosha suala hilo ili kuwachochea Waafrika wajenge dhana kwamba Mahakama ya ICC ni ya kibaguzi na udhalilishaji dhidi yao na kwamba ndio maana kesi za kina Kenyatta zinasikilizwa huko ughaibuni badala ya Kenya.
AU haitaki kuuambia ulimwengu na Waafrika kwamba kesi hizo zilipelekwa katika Mahakama hiyo iliyoko The Hague kutokana na Kenya kukataa kuunda mahakama ya kuendesha kesi dhidi ya Wakenya waliosababisha ghasia na vifo mwaka 2007. Inashangaza kuona mshikamano wa viongozi hao unakuja baada ya kugundua kwamba washtakiwa wakuu ni viongozi wenzao.
Ndio maana hawamwongelei mshtakiwa mwenzao, Joshua Arap Sang. Hofu yao inatokana na ukweli kwamba ICC ni kiboko cha watawala madikteta wanaotawala nchi zao kwa mkono wa chuma. Ndio maana viongozi hao wasiothamini haki za binadamu hivi sasa ndio vinara wa kuikashifu na kuidhalilisha ICC na kuchochea nchi wanachama wajitoe.
Ni jambo la kusikitisha kwamba Serikali ya Tanzania nayo imeingia kichwakichwa katika siasa hizo za mkumbo. Tangu nchi yetu ipate uhuru mwaka 1961, sera yake ya nchi za nje imekuwa ikiongozwa na msimamo wa kutofungamana na nchi yoyote katika masuala ya kipuuzi kama hili la kuikataa ICC, huku ikijua kwamba ilitia saini Mkataba wa Roma ulioanzisha Mahakama hiyo. Tungetegemea Rais Jakaya Kikwete atambue kwamba suala la Kenya kujitoa katika ICC limewagawa Wakenya vipandevipande, hivyo kuingilia suala hilo ni kuzidi kuwagawa. Rais pia anasahau kwamba Bunge la Kenya halikupata mwafaka wa kitaifa, bali lilitawaliwa na itikadi za kisiasa lilipoamua kuitoa nchi hiyo katika ICC.
Sisi tunasema Tanzania haina sababu ya kuiogopa ICC kama zilivyo baadhi ya nchi za Afrika. Pamoja na matukio ya hapa na pale, rekodi ya Serikali ya Tanzania katika masuala ya demokrasia na utawala bora kwa jumla ni nzuri. Tusisahau kwamba tutahatarisha fursa zetu kiuchumi kwa kutojipambanua kama nchi isiyoyumba katika kulinda haki za binadamu.