TFF tafuteni wadhamini ligi daraja la kwanza

Muktasari:

  • Ligi hiyo ya daraja la kwanza inatarajiwa kuwa na msisimko kwani zipo timu za African Lyon, Villa Squad, Majimaji, Lipuli, Toto Africa, Pamba na Polisi Dodoma ambazo ziliwahi kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom.

Ligi daraja la kwanza Tanzania Bara (FDL) inatarajiwa kuanza Septemba 14 mwaka huu, ambapo timu 24 zitapambana kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2014/2015.

Timu hizo zitakazoshiriki ligi hiyo ni Tasema United, African Lyon, Green Worriers, France Rangers, Villa Squad, Ndanda, Polisi Dar es Salaam na Trans Camp ambazo zipo kundi A.

Kundi B zipo Mkamba Rangers, Burkina Faso, Kimondo, Majimaji, JKT Mlale, Lipuli, Kurugenzi na Polisi wakati Kundi C zipo Toto African, Pamba, JKT Kanembwa, Polisi Mara, Polisi Dodoma, Polisi Tabora, Mwadui na Stand United.

Ligi hiyo ya daraja la kwanza inatarajiwa kuwa na msisimko kwani zipo timu za African Lyon, Villa Squad, Majimaji, Lipuli, Toto Africa, Pamba na Polisi Dodoma ambazo ziliwahi kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom.

Pia, msisimko mwingine unatokana na ukweli kuwa timu kama Pamba na Majimaji zinasaka nafasi ya kurudi Ligi Kuu mwakani ili kulinda heshima zao.

Hata hivyo, msisimko unaotarajiwa kuwapounaweza ukapotea kwa sababu hivi karibuni Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL), Silas Mwakibinga alisema wanahitaji Bilioni Moja na Milioni 38 kwa ajili ya kuendesha Ligi ya daraja la kwanza kwani haina udhamini.

Ni wazi timu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza hazina uwezo wa kifedha na hivyo zinakumbana na changamoto kubwa ya usafiri kutoka kituo kimoja kwenda kingine, pia zina matatizo ya kupata vifaa.

Sisi tunaona kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatakiwa kuifanyia kazi kauli ya Mwakibinga na kuifanyia kazi haraka kabla ya Ligi hiyo ya daraja la kwanza haijaanza mwezi Septemba.

Tunafahamu kuwa Ligi Kuu ina wadhamini ambao ni Vodacom, mashindano ya vijana chini ya miaka 20 yana wadhamini ambao ni Uhai, mashindano ya vijana chini ya miaka 17 yana wadhamini ambao ni Airtel nayale vijana chini ya miaka 15 yana wadhamini ambao ni Coca Cola.

Sasa sisi tunajiuliza inawezekana vipi TFF inashindwa kutafuta wadhamini kwa ajili ya ligi daraja la kwanza wakati haya ni mashindano muhimu yanayotafuta timu tatu zinazotakiwa kupanda Ligi Kuu kila mwaka?.

TFF wanatakiwa watambue kuwa Ligi daraja la kwanza ni ligi ya pili kwa ukubwa nchini baada ya Ligi Kuu kwa hiyo lazima iwe na udhamini wa maana.

Tunafahamu kuna makampuni mengi nchini ambayo yanataka kujitangaza kupitia mchezo wa soka kwani makampuni hayo ndiyo hunufaika zaidi kwa sababu mashindano ya soka huchezwa kwa muda mrefu.

TFF haitakiwi kukwepa jukumu hili la kutafuta udhamini wa Ligi daraja la kwanza kama kweli inataka kuona ligi hiyo inakuwa na msisimko na kukuza soka la Tanzania.

Tunasema hivyo kwa sababu jukumu la kukuza soka la Tanzania lipo chini ya TFF, lakini tunayashauri na makampuni mbalimbali kujitokeza na kuwania kuidhamini Ligi daraja la kwanza kwani ni fursa nzuri kwa makampuni kujitangaza kupitia ligi hiyo.

Tunafahamu kwamba zipo kampuni za simu, bima, vinywaji baridi, vinywaji vikali, mabenki na kampuni nyinginezo ambazo zinaweza kudhamini Ligi daraja lwa kwanza.

Sisi tunaamini TFF, Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL) na wadhamini ndiyo watakaofanya Ligi daraja la kwanza itakayoanza Septemba kuwa na msisimko kwani timu zitakazoshiriki ligi hiyo zimejiandaa na zinaendelea kujiandaa.