Kaze aanza na gia mpya Yanga

Muktasari:

  • Mastaa wote wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara wameitwa fasta Dar es Salaam ili kuwahi kambi inayoanza rasmi kesho Jumatatu na Kaze amesema sasa ni kazi tu, huku kiu kubwa ya mashabiki ni kuliona jembe lao jipya kutoka Burundi, Fiston Abdul Razack.

KOCHA wa Yanga, Cedrick Kaze alijifungia kwa siku kadhaa akikuna kichwa na sasa amesisitiza anaanza mazoezi kwa gia mpya kwa ajili ya mzunguko wa pili.

Mastaa wote wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara wameitwa fasta Dar es Salaam ili kuwahi kambi inayoanza rasmi kesho Jumatatu na Kaze amesema sasa ni kazi tu, huku kiu kubwa ya mashabiki ni kuliona jembe lao jipya kutoka Burundi, Fiston Abdul Razack.

Fiston amesajiliwa na Yanga kupitia dirisha dogo ili kuimarisha safu ya ushambuliaji wa timu hiyo ambayo inaongoza msimamo ikiwa na pointi 44, ikicheza mechi 18 bila kupoteza hata mchezo mmoja mpaka sasa.

Ligi Kuu iliyoyosimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021 na Fainali za Chan 2021 zinazoendelea nchini Cameroon, inatarajiwa kurejea tena Februari 13, lakini ikitanguliwa kwanza na mechi za viporo vya timu za Simba na Namungo.

Simba ina viporo vya mechi tatu dhidi ya Azam, Namungo na Dodoma Jiji, wakati wenzao wakiwa na michezo minne.

Katika kuhakikisha wanaendeleza moto ule ule waliouanza kwenye duru la kwanza na kwenda kuuendeleza Mapinduzi Cup kwa kutwaa ubingwa wakiwatungua watani wao, Simba kwa mikwaju ya penalti, mabosi wa Yanga wamewaita wachezaji wake kuwahi kambi.

Kwa mujibu wa Meneja, Hafidh Saleh kambi hiyo inaanza kesho Jumatatu na wachezaji tayari walishafahamishwa, lengo likiwa ni kujifua mapema baada ya kupewa mapumziko mafupi tangu walipotoka kwenye michuano ya Mapinduzi 2021.

“Kambi itaanza rasmi Jumatatu, Kigamboni na wachezaji wote wanayo taarifa,” alisema Hafidh ambaye hakutaka kufafanua zaidi.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli alisema wachezaji wanatarajia kuanza kuwasili leo kabla ya kesho kuanza mazoezi ya pamoja asubuhi na juu ya ujio wa Fiston ambaye ameziweka roho juu za mashabiki wa klabu hiyo, alisema naye ataiwahi kambi hiyo ya kesho.

“Fiston atawasili ndani ya siku hizo mbili, kwani awali kulikuwa na changamoto ya kupata ndege kumleta nchini, lakini tunaamini atawahi pamoja na wenzake kwenye kambi ya timu,” alisema Bumbuli.

Alipoulizwa juu ya wachezaji waliokuwa wakitajwa kama huenda wakapigwa chini, Michael Sarpong na Carlinhos, Bumbuli alisema wachezaji hao wamejaa tele na bado wapo sana Yanga na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kutosikiliza uzushi huo.

“Wachezaji wote wa kigeni wapo kikosini, hakuna aliyeachwa kwenye dirisha dogo, Fiston amekuwa kuiongezea nguvu safu yetu ya ushambuliaji iliyokuwa na kina Sarpong, Yacouba Songne na wenzao wengine, tunataka duru lijalo moto uwake maradufu,” alisema Bumbuli.

Fiston aliyewahi kukipiga LLB Académic, Rayon Sports, Diables Noirs, Sofapaka, Mamelodi Sundowns, Bloemfontein Celtic, 1º de Agosto, Al-Zawraa na JS Kabylie, anaungana na Saido Ntibazonkiza ambaye tangu atue Yanga ameuwasha moto akiifungia mabao mawili katika Ligi Kuu na kuasisti matatu, huku akifunga penalti ya mwisho katika derby iliyopigwa Mapinduzi.

Mbali na Fiston mchezaji mwingine aliyesajiliwa dirisha dogo ni beki wa kati Dickson Job kutoka Mtibwa, sambamba na wachezaji kadhaa kutoka timu ya Yanga U20.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali ilivyokuwa, Yanga huenda akaanzia mechi zake za Ligi jijini Mbeya kwa kuwafuata Mbeya City, baada ya awali kupata sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi yao ya kwanza ya duru la kwanza uliopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga Rukwa.