Mabao zaidi yatabiriwa Ligi Kuu

Wachezaji wa Yanga wakishangili bao la kwanza la mchezo dhidi ya Namungo katika uwanja wa Majaliwa, Lindi. Picha| Loveness Bernard.

Dar es Salaam. Kuna ongezeko la asilimia 14 ya mabao yaliofungwa katika mzunguko wa kwanza msimu huu, timu zikiwa zimefunga 260, ukitofautisha na msimu uliopita ambapo ngwe kama hiyo yalipachikwa 228, jambo linalotoa taswira ya kupatikana mengi zaidi.

Jumla ya mabao yote ya msimu wa 2021/22 yalikuwa 471, huku tayari msimu huu yakiwa yamefikiwa nusu yake, hilo linathibitisha namna msimu huu unavyoweza ukawa na idadi kubwa ya mabao.

Ukiachana na hilo, upepo umebadilika msimu huu, kwani Yanga ambayo hadi mzunguko wa kwanza unamalizika msimu uliopita ilikuwa kinara kwa mabao 25, msimu huu ni ya pili ikiwa 27.

Msimu uliopita, Simba ilikuwa nafasi ya tano kwa timu zilizopachika idadi kubwa ya mabao mzunguko wa kwanza, baada ya kufunga 16, lakini msimu huu ndiyo kinara wa kuzifumania nyavu (mabao 31).

Pamoja na klabu hizo kuchuana kwa kupishana kwa mabao, washambuliaji wao, Moses Phiri wa Simba anayecheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Bara ana mabao 10, sawa na Fiston Mayele wa Yanga, ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji wa pili kwa mabao 16, nyuma George Mpole wa Geita (17).

Kocha mzoefu, Kennedy Mwaisabula’ Mzazi alisema Ligi ya msimu huu inaweza kuwa na mabao mengi na hata kuvunjwa kwa rekodi ya mfungaji bora wa muda wote, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.