Manara bado pasua kichwa

Aliyekuwa Msemaji wa Yanga, Haji Manara alipowasili kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa katika kilele cha Wiki ya Mwananchi. Picha na Yanga

Muktasari:

  • Kitendo cha Manara kuonekana kwenye tukio la Wiki ya Mwananchi kimetafsiriwa na wanasheria kuwa hakuna kosa alilolifanya kutokana na kifungo alichopewa kutokuwa wazi ni namna gani hapaswi kujihusisha na masuala ya soka, hata kama shughuli ilikuwa ikihusisha sherehe za klabu ya soka.

ISHU ya Haji Manara bado ni pasua kichwa kutokana na kitendo chake cha kuibuka kwenye tamasha la Wiki ya Mwananchi kisha kusherehesha na kusepa zake huku akiwa kifungoni, kwani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kumpeleka tena kwenye Kamati ya Maadili kumshtaki.

Sio Manara tu, bali hadi Rais wa Yanga, Injinia Hersi naye kajumuishwa, huku wanasheria wakisema TFF imekurupuka kutoa uamuzi huo wa kumuingiza Injinia kwani yeye sio mtendaji wa klabu na baadhi yao wakigawanyika kwa Manara wengine wakiona amezingua kwa alichokifanya.

Kitendo cha Manara kuonekana kwenye tukio hilo kimetafsiriwa na wanasheria kuwa hakuna kosa alilolifanya kutokana na kifungo alichopewa kutokuwa wazi ni namna gani hapaswi kujihusisha na masuala ya soka, hata kama shughuli ilikuwa ikihusisha sherehe za klabu ya soka.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti walisema suala la Manara linapaswa kuwekwa wazi kwa kutolewa ufafanuzi kwani ni mwajiriwa wa Yanga na sio TFF, hivyo anaweza kutumika kwa namna nyingine yoyote tofauti na ilivyoainishwa kwenye ishu yake ya kufungiwa.

Mwanasheria Revocatus Kuuli alisema kama alitumika kwenye tamasha hilo kwa mwaliko maalumu na kulipwa kutokana na kazi aliyofanya hakuna makosa aliyoyafanya kwasababu amefungiwa kujihusisha na masuala ya kuizungumzia Yanga akiwa kama msemaji.

“Manara ni mwajiriwa wa Yanga, hivyo suala lake ni mtambuka anafanya kazi kama mwajiriwa hivyo yeye anaweza kuadhibiwa na mwajiri wake na sio TFF ili aweze kujua kipi hatakiwi kufanya unatakiwa uwazi wa hukumu yake,” alisema na kuongeza;

“Kama kaalikwa au kakodishwa kama MC kwa mkataba, hakuna makosa kwenye ishu hiyo, kifungo chake kilisema asijihusishe na kazi ya kuizungumzia Yanga na kwenda uwanjani kwake sio kosa ila anatakiwa kukaa katika majukwaa ya mashabiki sio sehemu ya viongozi.”

Wakili Aloyce Komba aliitaka TFF itoe ufafanuzi wa hukumu waliyoitoa kwa Manara ili aweze kufahamu ni vitu gani anatakiwa kufanya na kipi asifanye kwasababu hukumu yake haimzuii kutazama mpira bali ni kuuzungumzia.

“Pia Yanga ilipaswa kuvumilia kwa kipindi alichohukumiwa kumtumia ili kuepusha mambo kama yaliyotokea sasa japo sijafahamu anahukumiwa kwa kosa gani, jana ameshiriki kwa namna gani, MC? Je, alikuwa anazungumzia suala gani?” alihoji.

Alisema kama walimpatia nakala ya hukumu na kuainisha adhabu yake inamzuia maeneo yapi na kumpa nafasi ya kukata rufaa, kisha akakiuka, basi itamweka vibaya Manara.

“Kwa vile wanapelekwa Kamati ya Maadili tusubiri watazungumza nini, sina jambo jingine la kulizungumzia zaidi kwasababu suala tayari limeingia kwenye kesi,” alisema Komba, huku Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Kichere Mwita Waisaka alisema hana taarifa zozote juu ya kesi hiyo.

“Kama Mwenyekiti sina taarifa, zinaweza kuwa taarifa za mitandaoni tu, kumbuka hii ni wikiendi na kesho (leo) ni mapumziko ya sikukuu. Ila sijui chochote kwa sasa,” alisema Waisaka.

Manara alifungiwa kujihusisha na michezo kwa miaka miwili akitozwa pia faini ya Sh 20 milioni kwa tuhuma za kumtokea maneno makali Rais wa TFF, Wallace Karia katika fainali ya Kombe la ASFC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Yanga kubeba ubingwa kwa penalti.

Hata hivyo, hukumu hiyo imezua maswali kwa wadau kutokana na kamati kutomuita wala kumgusa Karia aliyejibishana na Manara na badala yake kamati inatumia ushahidi wa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao anayeiongoza Sekretarieti iliyomshtaki Manara na baadhi ya wanasheria wakahoji uhalali na kutaka itolewe ufafanuzi wa kutosha juu ya hukumu hiyo.


YANGA YAKOMAA

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema vigogo wa klabu hiyo wako nyuma na Ofisa Mhamasishaji wao Haji Manara katika uamuzi huo.

Bosi mmoja wa juu wa Yanga, aliliambia Mwanaspoti wana uhakika uamuzi wa TFF kupitia Kamati ya Maadili kumfungia Manara ulikuwa na maslahi ya kuikandamiza klabu yao na hata taarifa ya juzi ya kumshtaki tena yeye na Rais wa klabu hiyo, Injinia Said Hersi ni ukandamizaji uleule.

Bosi huyo alisema walikubaliana Manara apande jukwaani, kwa kazi yake kama MC na wala sio kiongozi wa Yanga.

“Nani asiyejua Manara hufanya hizi kazi za kusherehesha, sisi tulitaka akashereheshe na tunamlipa kwa kazi hiyo ni nje ya ajira yetu kama Mhamasishaji,” alisema bosi huyo (jina tunalo) na kuongeza;

“Hata wale washereheshaji wengine nao wana ajira zao nyingine lakini tunawalipa kwa kazi ile, ndio maana Manara alipomaliza kutambulisha wachezaji aliondoka zake kwenda kuitumikia adhabu yake.”

Kiongozi huyo aliongeza kutaka kuonyesha TFF ya sasa imekuwa ikiiandama Yanga ni jinsi ya kumbebesha kesi Injinia Hersi, kwani yeye sio Mtendaji na kuhoji TFF haijui majukumu ya Rais kikatiba wakati ilipitishwa na mamlaka zote na wao wakiwa na nakala.

“Hatutakubaliana na adhabu zozote safari hii, tunaona mengi ambayo yanafanyika kuikandamiza Yanga na unajua kama kuna kesi nyingi zilizohusisha klabu nyingine, lakini wameshindwa kuzitolea hukumu hadi sasa huku zikiwa na ushahidi wa wazi,” alisema kiongozi huyo.

“Kesi za Yanga zimekuwa zikitolewa hukumu haraka sana huku nyingine zikipigwa kalenda.”