Mastaa Prisons kuoga noti

UONGOZI wa Tanzania Prisons ukishirikiana na wadhamini wao wakuu, Kampuni ya Usafirishaji Silent Ocean umejipanga kuhakikisha mzunguko wa pili kikosi kinafanya vizuri kwenye michezo 15 na kumaliza Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa kwenye nafasi za juu.

 Uongozi wa Silent Ocean umeonyesha mfano kwa kutoa Sh10 milioni kwa wachezaji kama motisha iwapo watashinda michezo mitatu mfululizo kwenye ligi. Ahadi hiyo ni tofauti na pesa iliyotengwa kama bonasi ya kila mechi kutoka kwa uongozi.

Katika kuhakikisha kikosi hicho kinakuwa na matokeo mazuri uongozi wa timu hiyo umemwaga mkwanja kwa wachezaji wao ukiachana na ule uliyowekwa na wadhamini wao Silent Ocean, tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita au mzunguko wa kwanza.

Mzunguko wa kwanza wachezaji wa Prisons walikuwa wanapata bonasi ya Sh60,000 wakishinda mechi tofauti na Simba, Yanga, Azam na Mbeya City kwa sababu ni mchezo wa Dabi zinakutanisha timu mbili kutokea Mbeya.

Msimu uliopita na mzunguko wa kwanza wachezaji wa Prisons wakipata sare kwenye mchezo wao wowote nyumbani au ugenini walikuwa hawaambulii kitu.

Inaelezwa maboresho ya mzunguko wa pili kama Prisons itashinda wachezaji wote uwe umecheza au upo jukwaani na timu yao imeshinda kila mmoja anapata bonasi ya Sh100,000 katika mchezo wa nyumbani na ugenini.

Wachezaji wa Prisons kama watakuwa wametoka sare kwenye mchezo wowote watakuwa wanapata bonasi ya Sh60,000.

Taarifa hiyo inaeleza mechi dhidi ya Simba, Yanga, Azam na Mbeya City kama wakishinda kila mchezaji anavuta bonasi ya Sh200,000 na imekuwa nyingi tofauti na michezo mingine kutokana na ukubwa na ushindani wa timu hizo.

Alipotafutwa Ofisa habari wa Tanzania Prisons, Jackson Mwafulango alisema “Bonasi zipo kwa ajili ya kuwapa motisha wachezaji na si muhimu kuziweka wazi kwani ni makubaliano ya wachezaji na uongozi.”

Wakati bonasi zikiwa hivyo, Kocha wa Prisons, Patrick Odhiambo amesema bado ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kuwa timu yake inakaa kwenye njia imara kwenye michezo hii ya raundi ya mwisho.

“Bado tunahitaji kuongeza nguvu hasa katika mechi za nyumbani. Huu ni mzunguko wa pili, hivyo kila mechi tunatakiwa kuwa nayo makini ili kujiweka salama.

“Ukingalia mara nyingi mechi za ugenini huwa ni ngumu hivyo hata ukipata pointi moja unashukuru lakini nyumbani tunahitaji kujizatiti zaidi kuhakikisha tunashinda mechi nyingi kwenye mzunguko huu wa pili, ili kuwa katika nafasi nzuri na kuendelea kubaki kwenye ligi “alisema Odhiambo.

Tanzania Prisons katika duru la mzunguko wa kwanza ilifanikiwa kumaliza ikiwa katika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 15 wastani wa pointi moja kwenye kila mchezo iliyocheza.