Mayele amtibulia Rage kwa Simba

Mayele amtibulia Rage kwa Simba

TABORA. MABAO mawili yaliyowekwa kimiani na Fiston Mayele wa Yanga kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa juzi jijini Dar es Salaam yamemtibulia mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage aliyeitabiria timu yake ya zamani kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo ya dabi.

Rage aliitabiria Simba kushinda mabao 3-0, alipozungumza na wanachama wa Simba Tawi la Tumbi, mkoani hapa lakini Mayele alitibua baada ya kusawazisha bao la Pape Ousmane Sakho na kuongeza la ushindi katika kipindi cha pili.

Lakini wakati Rage akitibuliwa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Batilda Burian, saa chache kabla ya mchezo huo aliitabiria Yanga kushinda mchezo huo, ingawa hakutoa idadi ya mabao.

Akizungumza mapema juzi, RC Batilda aliwataka Wananchi wajiandae kupata furaha na kubeba Ngao, kwani mnyama ni lazima angekufa, jambo lililotokea kwenye kwenye Uwanja wa Mkapa.

“Nikitoka hapa naenda kuvaa jezi yangu mpya tayari kujiandaa kushuhudia mchezo huo kupitia runinga na kufurahia baada ya mchezo,” alinukuliwa RC huyo aliye shabiki wa kutupwa wa Yanga.