Mkude hana utani kazini

Monday August 01 2022
mkude pic
By Olipa Assa

KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude amesema kuzingatia majukumu yake uwanjani ni moja ya mambo yanayomfanya kocha asiache kumpanga kikosi cha kwanza.

Mkude alifichua alivyo ni tofauti na anavyochukuliwa na watu ni mtovu wa nidhamu na amesema ameamua kukaa kimya.

“Najua ninachotaka kwenye kazi yangu na uzuri wa soka ni mchezo wa wazi, hivyo kila mtu anakiona ninachokifanya. Ningekuwa sizingatii mazoezi, sidhani kama kuna kocha angependa kunitumia,” alisema na kuongeza;

“Soka linahitaji nidhamu ya juu ili kuwa na muendelezo wa kiwango, kikubwa najivunia kuwa sehemu ya Simba kwa muda mrefu kuliko mchezaji yoyote kwenye kikosi hiki.”

Alichosema kimekingiwa kifua na aliyekuwa kiungo wa Prisons, Lambart Sabiyanka kwamba staa huyo wa Simba uwanjani siyo mtu wa mchezo mchezo, tofauti na anavyochukuliwa na mashabiki nje.

“Ukiniambia nikutajie kiungo bora hapa Tanzania siwezi kuliacha jina la Mkude, jamaa ni fundi kweli kweli, hayo mambo yake ya nje hayanihusu, nazungumzia uwanjani anachokifanya,” alisema.

Advertisement

Mchezaji wa zamani wa Simba, Kasongo Athuman alisema yalivyo maisha ya Mkude ndivyo alivyokuwa zamani, kuna wakati mwingine alituhumiwa mambo asiyoyafanya, lakini aliekeleza nguvu zake kwenye kazi.

“Nilikuwa nasimamishwa mara nyingi kwenye timu, nikirudishwa napiga kazi, kilichokuwa kinaniponza nilikuwa nafuga rasta hivyo walikuwa wananichukulia kama mvuta bangi, ndio maana yapo mambo naweza kumkingia kifua Mkude, angekuwa hazingatii mazoezi basi asingedumu Simba muda wote huo, kwani wangapi walitokea kikosi B na hawapo,” alisema.

Mkude amedumu na Simba miaka 10 tangu alipopandishwa kutoka kikosi B mwaka 2012, hivyo ni mchezaji mkongwe zaidi ndani ya kikosi hicho, pia aliyecheza timu moja tu Ligi Kuu Bara.


Advertisement