Mpepo aliamsha mapema Namungo

Mpepo aliamsha mapema Namungo

LICHA ya kuwa Mtibwa Sugar, itaanzia ugenini kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Eliuter Mpepo anaamini kwa maandalizi waliyoyafanya watauanza msimu huu kwa ushindi tofauti na uliopita.

Msimu uliopita Mtibwa ilianza vibaya kwani ndani ya michezo yao mitano ya awali iliambulia pointi mbili tu kwa kutoka sare dhidi ya Tanzania Prisons na Geita Gold huku ikitandikwa na Mbeya Kwanza, Kagera Sugar na Dodoma Jiji.

Mpepo aliyetua Manungu kutokea Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja msimu uliopita, alisema kwa sasa mwelekeo wa Mtibwa ni mzuri hivyo mashabiki wa timu hiyo wategemee kuona utofauti kulingana na maandalizi waliyofanya chini ya kocha Salum Mayanga.

Mshambuliaji huyo alisema kila mchezaji kwenye kikosi chao anaonekana kuwa na ari ya kuipigania timu ili kurejea kwenye hadhi yake; “Sote tunajua Mtibwa ni moja ya timu kubwa hapa Tanzania, kilichotokea msimu uliopita hatupo tayari kuona kinajirudia tumekubaliana hilo na viongozi pamoja na benchi letu la ufundi.”

“Katika maandalizi yetu tumecheza michezo kadhaa ambayo benchi la ufundi iliona inatosha kutuweka sawa.Tutauanza msimu tukiwa ugenini, Namungo ni timu nzuri lakini tupo tayari kukabiliana nayo ili kuhakikisha tunauanza vizuri msimu,” alisema.