Namba za Mayele zatikisa

Dar es Salaam. Mabao mawili aliyopachika dhidi ya Dodoma Jiji juzi kwenye Uwanja wa Liti, Singida yamemfanya Fiston Mayele aongoze chati ya ufungaji Ligi Kuu msimu huu, lakini kwa upande mwingine yamemfanya atimize mambo manne ambayo ni nadra kutokea katika ligi yetu.

Mayele alifikisha idadi ya mabao nane wakati huo akitimiza jumla ya mabao 24 aliyofunga katika Ligi Kuu ukijumlisha 16 ya msimu uliopita.

Jambo la kwanza ni kubakiza idadi ya timu nne ambazo hajazifunga katika ligi kati ya 15 nyingine ambazo ni Simba, Tanzania Prisons, Mbeya City na Ihefu, huku zilizobakia (11) zikiwa zimeshawahi kuonja balaa la Mayele.

Mabao yake mawili aliyopachika dhidi ya Dodoma Jiji juzi, yameufanya mguu wake wa kulia kuendelea kuwa wa dhahabu zaidi kwake kwani ndiyo amekuwa akiutumia kufungia idadi kubwa ya mabao kulinganisha na wa kushoto na kichwa.

Kati ya mabao 24 aliyopachika katika Ligi Kuu, 17 amefunga kwa mguu wa kulia, huku moja tu akipachika kwa ule wa kushoto na sita yaliyobakia akifumania kwa kichwa.

Jambo lingine la kushangaza kwa Mayele ni kuwa tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu, ndiyo mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika mechi za ugenini (11) katika mechi tisa dhidi ya Mtibwa Sugar, KMC, Mbeya City, Biashara United, Coastal Union, Azam FC, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji na Geita Gold.

Mshambuliaji huyo amefungia mabao yake 24 katika viwanja tisa tofauti, ambavyo ni CCM Kirumba, Sheikh Anri Abeid, Majimaji, Sokoine, Liti, Benjamin Mkapa, Azam Complex, Manungu Complex na Mkwakwani.

Mayele ni balaa zaidi kipindi cha kwanza, kwani kati ya mabao 24 aliyofunga kwenye ligi, 15 ameyapata dakika 45 za kwanza.

Amefunga bao katika kila robo ya mchezo kati ya sita za dakika 90, na amekuwa hatari zaidi katika robo ya tatu, ambayo ni dakika ya 31 hadi ya 45, katika muda huo amepachika nane.

Kocha wa zamani wa Mbeya City na Tanzania Prisons, Adolf Rishard alisema kikubwa kinachombeba Mayele ni kujitambua na kufanya kazi yake kwa ufasaha tofauti na wengine.

“Yuko ‘serious’ na anachokifanya ndiyo maana anafanikiwa na kuisaidia timu yake kufanya vizuri hadi sasa, hii ndio maana ya mchezaji ‘Professional’ (anayelipwa) lazima ajitofautishe,” alisema Rishard.

Aliyekuwa kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza anasema Mayele ni mchezaji anayejieleza na kitu kikubwa anachofanikiwa kwa kiasi kikubwa nyota huyo ni kujituma na kuwa na uchu wa mafanikio.