Presha ugenini yazidi Simba

Mbeya. Simba imejiongezea presha katika michezo yake minne ijayo ya Ligi Kuu ya ugenini, baada ya jana kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, mabingwa wa zamani walitangulia kupata bao la kuongoza dakika ya 15 kupitia kwa kiungo Mzamiru Yassin, kabla ya Tariq Seif kuisawazishia Mbeya City kipindi cha pili.

Hii inakuwa sare ya tatu ya Simba msimu huu, ikiacha nafasi kwa Yanga kujiimarisha kileleni, kwani ina mechi mbili mkononi huku Simba ikiachwa kwa pointi moja.

Licha ya kuwa na nyota wake Clatous Chama, Augustine Okrah na John Bocco, Simba haikuwa na mbinu kipindi cha pili cha kuzuia kasi ya Mbeya City.

Hofu zaidi kwa mabingwa hao wa zamani ni kutokana na kuwa na mechi mfululizo za ugenini, kwani itasafiri kuifuata Polisi Tanzania (Jumapili), kisha kwenda Mkwakwani kuikabili Coastal Union (Desemba 3). Itasafiri kuifuata Geita Gold jijini Mwanza.

Kocha wa Simba, Juma Mgundu alisema ni matokeo mabaya lakini walikutana na timu ngumu (Mbeya City), hivyo wana kila sababu ya kubadilika katika michezo ijayo.