Rekodi kumbeba Mwakinyo leo

Muktasari:

Wakati dakika 36 za raundi 12 zikisubiriwa kuamua bingwa wa mabara wa WBF kati ya Hassan Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina, uzoefu na rekodi ndivyo vitu ambavyo vinawatofautisha mabondia hao wenye nyota sawa kwenye renki ya dunia.

Dar es Salaam. Wakati dakika 36 za raundi 12 zikisubiriwa kuamua bingwa wa mabara wa WBF kati ya Hassan Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina, uzoefu na rekodi ndivyo vitu ambavyo vinawatofautisha mabondia hao wenye nyota sawa kwenye renki ya dunia.

Mabondia hao wanapanda ulingoni leo kuzichapa kuwania mkanda wa mabara wa WBF, pambano litakalochezeshwa na refarii wa kimataifa, Edward Marshal na kusimamiwa na rais wa WBF, Goldberg Howard kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Dar es Salaam.

Mwakinyo bondia namba moja nchini atakuwa nyumbani kutetea ubingwa huo alioshinda Agosti mwaka huu alipomchapa Tshibangu Kayembe wa DR Congo, pambano linalotazamwa kuamuliwa na uzoefu wa Paz na rekodi za Mwakinyo.

Jana mabondia hao wenye nyota mbili na nusu kila mmoja walipima uzito na afya tayari kuzichapa, huku Mwakinyo akitambia rekodi ya kushinda mfululizo tangu 2018 alipomchapa Sam Egginton nchini Uingereza hadi sasa huku Paz tangu mwaka huo ameshinda mara moja na kupigwa kwenye mapambano manne mfululizo.

Mbali na Kayembe na Eggingto, Mwakinyo amemchapa Arnel Tinampay, Said Yazidu, Eduardo Gonzalez na Joseph Sinkala.

Paz yeye atapanda ulingoni akijivunia uzoefu, licha ya kuchapwa mapambano manne mfululizo mawili ikiwa kwa KO, pointi na TKO na kushinda moja kwa TKO, ni mzoefu karibu mara mbili ya Mwakinyo.

Bondia huyo anayenolewa na baba yake mzazi amecheza mapambano 35 na kushinda 23, amepigwa mara 11 na kutoka sare pambano moja, wakati Mwakinyo amecheza mapambano 19 pekee na kushinda 17.

Jana mabondia hao walitambiana kwenye zoezi la kupima uzito na afya lililoshuhudiwa pia na mwamuzi wa kimataifa, Edward Marshal na Rais wa WBF, Goldberg Howard.