Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Serikali: Hakuna muda wa nyongeza miundombinu uwanja wa AFCON

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuelekea uwanja wa kuzunguka uwanja wa AFCON, jijini Arusha leo Ijumaa Machi 20, 2026.

Muktasari:

  • Serikali imesema kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Juni 2027, ambapo miundombinu hiyo inapaswa kukamilika Mei 2027 na kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza

Arusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, amemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara kuelekea na kuzunguka uwanja utakaotumika katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027 Arusha, kuhakikisha anakamilisha kwa wakati mradi huo kwani hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Amesema anapaswa kumaliza mradi huo kwa wakati, ili kuiwezesha Tanzania kuwa tayari kwa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Juni, 2027.

Profesa Shemdoe ametoa maelekezo hayo Ijumaa Machi 20, 2026 wakati akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuelekea uwanja na kuzunguka uwanja huo.

Amesema mradi huo utakaoanza Aprili Mosi mwaka huu unatarajiwa kukamilika Mei 2027 na kusisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa wahandisi kuhakikisha kila hatua ya utekelezaji inafuata ratiba.

“Nitakuwa ‘serious’ kwenye usimamizi huu, hatutaruhusu uzembe wowote katika utekelezaji wa mradi huu muhimu kwani hatutaki maombi ya nyongeza maana mashindano yataanza Juni hivyo lazima ukamilike Mei 2027," amesema

Profesa Shemdoe amesema kutokana na ukubwa wa mashindano hayo, dunia yote itaelekeza macho yake Tanzania wakati wa mashindano hivyo ni fursa ya kuonesha uwezo wa nchi katika miundombinu na maandalizi ya matukio yote.

"Barabara zilizo chini ya Tarura zina mchango mkubwa wa ukuaji wa ustawi wa uchumi na zinagusa wananchi moja kwa moja. Barabara hizi hazitaondoka na AFCON. Mashindano yatakapomalizika moja ya vitu vikubwa tutakavyoachiwa ni barabara hizi," amesema.

Hafla ya utiaji saini mkataba wa uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuelekea uwanja wa AFCON Arusha.

Waziri huyo amewaomba wananchi kuwa wasimamizi wa miradi hiyo na kulinda miundombinu hiyo wakati na baada ya kukamilika kwake na kuendelea kutoa ushauri na maoni yao katika kuunga mkono juhudi za serikali kwa moyo wa uzalendo.

Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura),Mhandisi Victor Seff, amesema mradi huo utagharimu zaidi ya Sh82.9 bilioni ambapo kati ya hizo Sh81.5 bilioni ni gharama za usanifu wa kina na ujenzi kwa mkandarasi na Sh1.408 bilioni ni gharama za mshauri elekezi za usanifu wa awali na kutayarisha mahitaji ya mwajiri.

Amesema mradi unatekelezwa na kampuni ya M/s China Railway Construction Engineering Group, ambao utasimamiwa na Mhandisi Mshauri, kampuni ya M/s Afrisa Consulting LTD ya Dar Es Salaam.

Amesema kutakuwa na gharama za fidia kwa wananchi watakaoathirika na ujenzi huu ambapo mradi wote unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

Amesema ujenzi wa uwanja huo unaoendelea kujengwa ambao umefikia zaidi ya asilimia 75 na kuwa sambamba na ujenzi huo wa uwanja ujenzi wa miundombinu muhimu ya barabara yenye jumla za kilomita 19.9 kwa kiwango cha lami kuelekea kwenye uwanja kutokea barabara kuu za Arusha – Babati na Arusha Bypass na kuzunguka uwanja.

Ametaja barabara hizo ni Mateves - Bondeni kilomita 6.5 na kati ya hizo kilomita 1.5 njia nne na kilomita 5 njia mbili,nyingine ni kutoka barabara kuu ya Arusha – Babati, barabara ya Lendita kilomita 2.75 njia nne, barabara ya Essuri kilomita 2.45 njia nne zote kutoka barabara kuu ya Arusha bypass na kilomita 1.5 barabara kuzunguka uwanja.

"Kwa mujibu wa usanifu wa awali, masuala mtambuka kama vile masuala yanayohusu mazingira, uhusiano wa jamii, matumizi ya teknolojia yamepewa umuhimu kwa Mkandarasi kuyazingatia ili kuweza kuleta ufanisi wa Mradi na hatimaye kuendana na dhamira ya Serikali katika kujenga miundombinu endelevu, jumuishi na yenye kuhimili Mabadiliko ya tabia nchi ," amesema

Mtendaji huyo ametaja barabara za Lendita,Essuri na kipande cha kilomita 1.5 barabara ya Mateves zitajengwa kwa njia nne zinazojumuisha upana wa barabara mita saba na mabega mita 0.9 kwa kila upande na 'median' ya mita tisa,pamoja na eneo la upana wa mita mbili kwa ajili ya usalama wa watembea kwa miguu na vyombo visivyo vya moto.

Amesema kipande cha kilomita tano barabara ya Mateves kitajengwa kwa njia mbili zenye upana wa mita saba,mabega mita moja kila upande na daraja moja la upana wa mita 100 la zege litakalojengwa barabara ya Essuri.

"Kutawekwa taa za barabarani zinazotumia nishati ya jua,alama zote muhimu za usalama barabarani zitawekwa ikiwa ni pamoja na mistari ya kwenye alama. Mradi utatekelezwa kwa muda wa miezi 13," amesema

Awali Waziri wa Habari,Sanaa,Utamaduni na Michezo, Paul Makonda amesema  barabara ni kipaumbele na kama kuna jambo wananchi hawatofautiani ni miundombinu ya barabara.

Amesema kushuhudiwa kwa utekelezaji wa mradi huo moja kwa moja unaongeza imani na faraja kwa jamii na kuwa wananchi wamekuwa wakiteseka na changamoto ya miundombinu.

"Uwanja wa AFCON hauwezi kufikika kama barabara ni mbovu na ugeni ni mkubwa. Dunia yote macho yatakuwa Tanzania na mji wa Arusha na kwa upekee wa Arusha itakuwa na fursa nyingi kutumia mashindano kujenga uchumi wake,” amesema Makonda.

Amesema kuwa barabara hizo zitakwenda kuungana na barabara zingine na kufungua mkoa huo na kuomba kuongezwa barabara zingine za lami ikiwemo kutoka Philips-Impala hadi Njiro ambayo imekuwa na msongamano mkubwa na kuwa ujenzi wa barabara mbili na nne zitasaidia kupunguza barabara kufungwa pindi kunapokuwa na mikutano mikubwa.