Simba yazua balaa

Monday November 23 2020
simba pic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Uongozi wa Coastal Union umepanga kuchukua hatua za kinidhamu kwa wachezaji wao baada ya kipigo cha juzi cha mabao 7-0 dhidi ya Simba.

Coastal Union ilikubali kipigo hicho ambacho ni kikubwa kutokea tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, huku uongozi ukisisitiza kimetokana na nidhamu mbovu.

“Wachezaji wetu hawajielewi, hawakufanya mazoezi na ndiyo chanzo cha matokeo hayo,” alisema Mwenyekiti wa Coastal, Steven Mguto, ambaye alikuwa Arusha kwenye mchezo huo, ambao Coastal Union ilitumia Uwanja wa Shehk Amri Abeid, Arusha, kama uwanja wao wa nyumbani baada ya ule wa Mkwakwani, Tanga kufungiwa.

Mguto alisema timu haikuwa na maandalizi ya mechi hiyo na hiyo imetokana na uzembe wa wachezaji wenyewe.

“Walipewa mapumziko ya siku tatu wakati Ligi imesimama, lakini wengi wao hawakurudi kwa wakati, wengine wamerudi siku moja kabla ya mechi,” alisema.

Alisema ukumbwa wa mechi na Simba na maandalizi waliyoyafanya havikuendana na ndiyo chanzo cha kipigo hicho.

Advertisement

“Tumeyakubali matokeo, ila tutaangalia cha kufanya kwenye hili, kuna wachezaji tutawachukulia hatua za kinidhamu,” alisema Mguto.

Simba ambayo Ijumaa ijayo itakuwa ugenini kucheza mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Plateau United imesema ushindi huo ni moja ya kipimo kizuri kwao kabla ya kuelekea Nigeria kesho.

Katika mchezo huo, Simba ilikuwa na mabadiliko machache, wakati mkongwe Erasto Nyoni akirejea kikosini kucheza nafasi ya Jonas Mkude na Benard Morrison akianza na kufunga bao.

Said Ndemla aliendeleza kiwango chake bora tangu kuanza kupata nafasi katika kikosi cha Simba msimu huu, akiaminika kuichezesha timu na nahodha John Bocco akifunga hat trick ya pili kwenye Ligi Kuu msimu huu. Awali ilikuwa ya Adam Adam JKT Tanzania alipoifunga Mwaduni.

Kocha Sven Vandenbroeck alisema ushindi huo mnono umekuwa chachu kwao na anaamini wataendelea na rekodi hiyo kwenye mechi zijazo ikiwamo ya Ligi ya mabingwa.

Simba itaondoka Jumatano na msafara wa watu 40 kuelekea Nigeria tayari kwa mechi hiyo muhimu ya mzunguko wa awali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji alisema watatumia ndege ya kukodi kutoka Lagos kwenda mjini Jos.

“Lengo la klabu msimu huu ni kufika mbali, kwa miakati tuliyoiweka na maandalizi tunayoyafanya tunaamini tutatimiza malengo yetu na kufanya vizuri kimataifa,” alisema Mo.

Mbali na mechi hiyo, KMC juzi iliiduwaza Azam kwa kuifunga bao 1-0, matokeo yaliyoifanya Azam kufungwa mechi ya pili msimu huu.

Katika mchezo uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, wenyeji Kagera Sugar iliibuka na ushindin wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga.

Advertisement