Vunjabei afunguka hasara ya jezi mpya Simba

Vunjabei apata hasara Simba

WAKATI wanachama na mashabiki wa Simba wakianza kusahau machungu ya pilikapilika za kugombea jezi mpya za klabu hiyo, mwenye dili na uzi za Simba, Fred Ngajiro ‘Vunjabei, amevunja ukimya na kufichua hasara ya kupoteza Dola 150,000 (zaidi ya Sh349 milioni).

Vunjabei alisema hasara hiyo imetokana na kubadilisha mfumo wa jezi za awali baada ya kubadilishwa kwa mdhamini kutoka SportPesa na kuwa M-Bet.

Mfanyabiashara huyo alisema, mkataba mpya ulipokuja alikuwa ameshadizaini jezi za mdhamini wa awali, hivyo kumtia hasara ya kiasi hicho cha fedha za kuweka mdhamini mpya.

“Simba waliponipigia simu kuniambia juu ya kusitisha uzalishaji wa jezi kutokana na mkataba mpya basi ikanibidi na mimi nipige simu zoezi lisitishwe jambo ambalo limefanya jezi zichelewe,” alisema Vunjabei na kuongeza;

“Mkataba na mdhamini wa sasa ulikuwa mzuri na ndio maana tuliamua kutulia ili kuzungumza na kuweka mambo sawa kwa kuwa zile ni pesa za wanasimba, kitendo cha kukurupuka kisa mkataba una pesa ndefu halafu mkaharibu sio sawa.”

Vunjabei alisema athari ya kuchelewa kwa jezi ni kitendo cha wanasimba kukwazika lakini hakuwa na namna aliona ni bora kuchelewa kuvaa jezi halafu mkataba ukawa mzuri.

Uzi huo mpya ulichelewa kutambulishwa na hata uliopotolewa hadharani haukupatikana kirahisi na kuwakera mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, lakini uongozi ulishatoa ufafanuzi mapema.

“Hata mimi niliumia jezi kuchelewa, usafirishaji umekuwa shida kubwa kutokana na mambo mengi kwa sasa lakini kuanzia jumatatu jezi zitakuwa zimefika na meli,” alisema Vunjabei.

Alisema mkataba wa jezi za Simba umemfanya jina lake kuzidi kuwa kubwa hivyo hata kitendo cha kupata hasara hiyo ya matayarisho ya awali hakuona shida na aliamua kukaa kimya.