Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

56 wafariki dunia vurugu kwenye mechi ya mpira wa miguu

Muktasari:

  • Mechi hiyo ilikuwa sehemu ya mashindano ya kumheshimu kiongozi wa kijeshi Mamady Doumbouya, anayekabiliwa na ukosoaji wa mpango wake wa kugombea urais, kinyume na ahadi ya kurejesha utawala wa kiraia ifikapo mwishoni mwa 2024.

Guinea. Watu 56 wamepoteza maisha baada ya ghasia zilizotokea kwenye mechi ya mpira wa miguu katika mji wa N’Zerekore, kusini-mashariki mwa Guinea.

Tovuti ya Aljazeera leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 imeandika kuwa ripoti zinaonyesha tukio hilo lilianza baada ya mwamuzi kuwapa kadi nyekundu wachezaji wawili wa timu ya wageni (Labe) na kuamuru penalti yenye utata.

Malalamiko yaliyotoka kwa wachezaji wa timu ya Labe kuhusu uamuzi wa mwamuzi huyo yaliyosababisha mashabiki wa timu hiyo kurusha mawe, hivyo kusababisha vurugu. Polisi wamelazimika kuingilia kati jambo hilo kwa kuwarushia mabomu ya machozi na kusababisha watu kukimbia kwenye njia moja na kusababisha vifo hivyo.

“Mambo yote yalianza baada ya kupingwa uamuzi wa mwamuzi, kisha mashabiki wakaingia uwanjani,” amesema shahidi mmoja akilieleza Shirika la Habari la Ufaransa (AFP).

Waziri Mkuu, Oury Bah, katika taarifa yake amesema uchunguzi umeanzishwa ili kuwabaini waliohusika kuanzisha vurugu hizo.

Pia ametoa rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao, huku akiahidi msaada wa matibabu na kisaikolojia kwa waliojeruhiwa.

Mechi hiyo ilikuwa sehemu ya mashindano yaliyoandaliwa kwa heshima ya kiongozi wa kijeshi wa Guinea, Mamady Doumbouya aliyetwaa madaraka mwaka 2021 kupitia mapinduzi.

Mashindano kama hayo ya soka kwa heshima ya kiongozi wa kijeshi yaliandaliwa sehemu nyingine nchini na wapinzani wakiyalaumu ni mbinu ya kumuunga mkono Doumbouya kwa uchaguzi ujao.

Doumbouya alitwaa madaraka kwa nguvu Septemba 2021, akimuondoa Rais Alpha Conde ambaye awali alimemteua kuwa kiongozi wa kikosi maalumu cha ulinzi wa Rais, chini ya shinikizo la kimataifa. Doumbouya aliahidi kurudisha madaraka kwa Serikali ya kiraia ifikapo mwishoni mwa 2024, lakini tangu wakati huo ameweka wazi kuwa hatofanya hivyo.

Januari 2024, Doumbouya alijipandisha cheo kuwa Luteni Jenerali na mwezi uliopita akajipandisha cheo tena na kuwa Jenerali wa Jeshi.

Ingawa katiba ya mpito iliyoandaliwa baada ya mapinduzi ilieleza hakuna mwanajeshi anayeruhusiwa kugombea katika chaguzi za kitaifa au za mitaa, wafuasi wa Doumbouya hivi karibuni wameonyesha kumuunga mkono kugombea urais

Mwishoni mwa Septemba 2024, mamlaka zilionyesha uchaguzi uliokusudiwa kurejesha utawala wa kikatiba utafanyika mwaka 2025.