Afcon 2023 ilivyoacha rekodi tamu

Muktasari:

 Rekodi mbalimbali zimewekwa katika fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizomalizika juzi huko Ivory Coast ambapo mwenyeji iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Nigeria.

Rekodi mbalimbali zimewekwa katika fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizomalizika juzi huko Ivory Coast ambapo mwenyeji iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Nigeria katika mchezo wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Alassane Ouattara jijini Abidjan.

Ni mashindano yaliyopelekea rekodi mbalimbali mpya kuwekwa na nyingine kufikiwa ama na wachezaji binafsi au timu.

Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya rekodi ambazo zimefikiwa au kupitwa kupitia fainali za Afcon zilizomalizika juzi.

Fae na alama yake

Kwa kuiongoza Ivory Coast kutwaa ubingwa wa Afcon, Emerse Fae anakuwa kocha wa kwanza mzawa kuipa taji hilo kubwa nchi hiyo, kwani mara mbili zilizopita ambapo ilitwaa ubingwa, ilikuwa ikinolewa na makocha wa kigeni.

Mwaka 1992, Ivory Coast ilikuwa chini ya kocha Radivoje Ognjanović aliyekuwa akitokea Yugoslavia na ilipotwaa ubingwa mwaka 2015 ilikuwa inanolewa na Hervé Renard.

Williams mikono ya dhahabu

Kipa wa Afrika Kusini, Ronwen Williams alimaliza mashindano hayo akibeba tuzo ya kipa bora lakini hilo halikutokea kwa bahati mabaya na badala yake alivuja jasho hadi kupelekea kuondoka na tuzo hiyo.

Miongoni mwa mechi ambazo Ronwen Williams alionyesha kiwango bora ni ile dhidi ya Cape Verde ambayo mbali na kuokoa hatari nyingi alizoelekezewa na baadaye kugeuka shujaa katika upiganaji wa penalti katika kumsaka mshindi ambapo aliokoa penalti nne kwa mpigo na kuiwezesha timu yake kupata ushindi wa penalti 2-1.

Kwa hilo alilofanya, WilliAms aliweka rekodi ya kuwa kipa wa kwanza katika historia ya Afcon kuokoa penalti nne katika mechi moja.

Mabao ya kumwaga

Fainali za mwaka huu zimeweka rekodi ya kuwa na idadi kubwa ya mabao kuliko nyingine zote za nyuma ambapo idadi ya mabao 119 yalifungwa katika michezo 52 ikiwa ni wastani wa mabao 2.9 kwa mechi.


Idadi hiyo inavunja rekodi ya mabao yaliyofungwa katika fainali za Afcon 2019 ambapo idadi ya mabao 102 yaliwekwa kimiani sawa na wastani wa bao 1.96 kwa mechi.

Tanzania ilipokata mnyororo wa unyonge

Timu ya taifa ya Tanzania ilishiriki kwa mara ya tatu katika fainali hizo ambapo ilijikuta ikimaliza mkiani mwa kundi F baada ya kukusanya pointi mbili katika mechi tatu ilizocheza dhidi ya Morocco, Zambia na DR Congo.

Ilikuwa ni mwendelezo wa kumaliza ikiwa ya mwisho kwenye hatua ya makundi lakini ilifanikiwa kuvunja rekodi yake ya kupata pointi nyingi zaidi katika mashindano hayo kwani haikuwahi kumaliza na pointi zaidi ya moja iliposhiriki hapo kabla.

Katika fainali zake za kwanza kushiriki mwaka 1980, Taifa Stars ilimaliza Afcon ikiwa na pointi moja na mwaka 2019 haikuambulia pointi yoyote baada ya kupoteza mechi zote tatu kwenye kundi lake.

Mauritania rekodi mbili

Ikiwa inashiriki kwa mara ya tatu kwenye fainali za Afcon, timu ya taifa ya Mauritania ilijiwekea rekodi zake mbili ambazo pengine zimesaidia kuishawishi irefushe mkataba wa kocha wake Amir Abdou kwa miaka miwili zaidi hadi 2026.

Rekodi ya kwanza ni kupata ushindi wa kwanza kwenye Afcon baada ya kuichapa Algeria kwa bao 1-0 katika hatua ya makundi na rekodi ya pili ni kutinga hatua ya 16 bora ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza.