Afrika Kusini yatinga 32 bora Kombe la Dunia
Muktasari:
- Matokeo hayo yanaifanya Bafana Bafana kumaliza nafasi ya pili katika kundi A ikiwa na pointi nne nyuma ya Mexico yenye pointi tisa, huku Korea Kusini ikiwa ya tatu na pointi tatu wakati Czech ikiburuza mkia kwa pointi moja.
Monterrey, Mexico. Bao la dakika ya 63 la nyota wa Afrika Kusini, Thelapo Maseko dhidi ya Korea Kusini limetosha kuipeleka hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia ikiingana na wenyeji, Mexico, waliomaliza vinara wa kundi A.
Mechi hiyo ya kundi A iliyopigwa kwenye Uwanja wa BBVA, uliopo mjini Guadalupe katika Jimbo la Nuevo Leon Kaskazini mwa Mexico, iliichukua Afrika Kusini dakika 63 kuihakikishia timu hiyo kusonga hatua ya mtoano.
Matokeo hayo yanaifanya Bafana Bafana kumaliza nafasi ya pili katika kundi A ikiwa na pointi nne nyuma ya Mexico yenye pointi tisa, huku Korea Kusini ikiwa ya tatu na pointi tatu wakati Czech ikiburuza mkia kwa pointi moja.
Katika hatua ya 32 bora, Afrika Kusini itakutana na wenyeji Canada waliomaliza nafasi ya pili kundi B, mechi itakayopigwa Juni 28, 2026.
Afrika Kusini inashiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya nne baada ya kushiriki mara ya kwanza 1998 nchini Ufaransa, ambapo iliishia hatua ya makundi nyuma ya Ufaransa, Denmark na Saudi Arabia.
Katika kundi C, Ufaransa ilimaliza kinara na pointi tisa nyuma ya Denmark iliyokuwa ya pili na pointi nne, huku Afrika Kusini ikiwa ya tatu na pointi mbili, wakati Saudi Arabia iliburuza mkiani na pointi moja.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2002 lililofanyika Korea Kusini na Japan, Afrika Kusini iliishia pia hatua ya makundi na sasa imeingia mtoano kwa mara ya kwanza huku ikikumbukwa zaidi 2010 ilipokuwa taifa la kwanza kutoka Afrika kuandaa fainali za Kombe la Dunia.
Kwa upande wa Korea Kusini imekuwa miongoni mwa timu za Asia zilizoshiriki fainali hizo mara nyingi zaidi kuanzia 1954, nchini Uswisi na mafanikio makubwa ni kufika nusu fainali 2002.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2002, Korea Kusini ilikuwa mwenyeji kwa kushirikiana na Japan ambapo ilikuwa ni timu ya kwanza ya Asia kufika nusu fainali iliyopoteza kwa kuchapwa na Ujerumani bao 1-0, Juni 25, 2002.
Mafanikio mengine makubwa ni kushiriki mara 11 mfululizo kuanzia 1986 hadi 2026, huku nafasi bora zaidi ni kumaliza ya nne 2002 ilipokuwa mwenyeji, wakati 2010 na 2022 iliishia hatua ya 16 bora.