Ahoua, Pacome tumaini la Simba, Yanga ugenini
Dar es Salaam. Takwimu bora za kushambulia za viungo Jean Charles Ahoua wa Simba na Pacome Zouzoua wa Yanga zinawafanya wawe silaha muhimu kwa Simba na Yanga kesho Jumapili timu hizo zitakapokuwa ugenini katika nchi za Angola na Mauritania kucheza mechi za raundi ya tano ya mashindano ya klabu Afrika.
Kuanzia saa 4:00 usiku, Yanga itakabiliana na Al Hilal ya Sudan katika Uwanja wa Cheikha Ould Boïdiya jijini Nouakchott, Mauritania ikihitaji ushindi ambao utaweka hai matumaini yake ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kabla ya mchezo huo, Simba itakuwa ugenini jijini Luanda, Angola katika Uwanja wa Novemba 11 kukabiliana na Onze Bravos Marquis ikihitaji ushindi wa aina yoyote iweze kutinga hatua ya robo fainali, ingawa pia sare kwenye mchezo huo inaweza kuivusha Simba ikiwa CS Constantine itapata ushindi dhidi ya CS Sfaxien.
Wakati Al Hilal na Bravos zikionekana kuwa na rekodi nzuri ya ubabe nyumbani katika mechi za kimataifa, muendelezo wa ubora ambao Pacome na Ahoua wamekuwa nao katika ujenzi wa mashambulizi kwenye mechi za kimataifa hapana shaka unaziweka Yanga na Simba katika imani ya kutikisa ugenini kwa kufanya vizuri katika mechi hizo.
Wakati Pacome akiwa tishio zaidi katika kikosi cha Yanga kwa kutengeneza nafasi za mabao kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ahoua ni hatari kwa kutengeneza nafasi, kufunga na hata kupiga pasi za mwisho kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa mujibu wa mtandao wa fotmob.com, Pacome ndiye mchezaji wa Yanga aliyetengeneza nafasi nyingi katika mechi nne za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa nazo nane, sawa na wastani wa nafasi mbili kwa mchezo akifuatiwa na Aziz Ki Stephane ambaye ametengeneza nafasi saba.
Hata hivyo bahati mbaya ya Pacome ni kwamba nafasi hizo zote nane alizotengeneza, hazijaweza kubadilishwa kuwa mabao.
Ahoua kwa upande wake ndio kinara wa kutengeneza nafasi katika kikosi cha Simba akiwa amefanya hivyo mara tisa na kiujumla anashika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo nyuma ya kinara Yassine Labhiri wa RS Berkane aliyefanya hivyo mara 14.
Ahoua ndiye kinara wa kufumania nyavu katika kikosi cha Simba kwenye mashindano hayo akifunga mabao mawili sawa na Kibu Denis, lakini pia ndiye anaongoza kwa kupiga pasi za mwisho akiwa nazo mbili.
Kwenye mashindano hayo, Ahoua ndiye kinara wa kupiga pasi za mwisho na anashika nafasi ya pili kwa kuhusika na idadi kubwa ya mabao akifanya hivyo katika mabao manne huku kinara akiwa ni Ismail Belkacemi wa USM Alger akiwa amehusika na mabao sita.
Beki wa zamani wa Yanga na Simba, Bakari Malima alisema kuwa Ahoua na Pacome wanastahili kupongezwa kwa namna wanavyotoa mchango kwa timu zao kwenye mashindano hayo.
"Mchezaji wa kimataifa anapoletwa anatakiwa kuonyesha thamani yake kwenye mechi za kimataifa kama wanavyofanya Pacome na Ahoua. Ni wachezaji muhimu ambao wakiendelea kuwa na viwango vyao, watazisaidia sana Simba na Yanga," alisema Malima.