Aliyechukua nafasi ya Palmer ana balaa
Muktasari:
- Kocha Maresca alisema Palmer alipata maumivu ya kinena wakati anapasha misuli moto muda mfupi kabla ya mechi hiyo kuanza na alikuwamo kwenye kikosi kilichopaswa kuanza kabla ya kuchomolewa na kupewa nafasi Estevao.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca ameelezea kilichomfanya Cole Palmer kushindwa kucheza mechi ya West Ham United, huku mchezaji aliyecheza badala yake, Estevao Willian akionyesha balaa kubwa uwanjani.
Kocha Maresca alisema Palmer alipata maumivu ya kinena wakati anapasha misuli moto muda mfupi kabla ya mechi hiyo kuanza na alikuwamo kwenye kikosi kilichopaswa kuanza kabla ya kuchomolewa na kupewa nafasi Estevao.
Staa huyo, Estevao alionyesha kiwango matata kabisa uwanjani, wakati Chelsea ilipotokea nyuma kwa bao 1-0 na kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 ugenini.
Ushindi huo mnono umeondoa presha kwamba Chelsea inaweza kushinda na kuvuna pointi bila ya kuwa na huduma ya kiungo huyo mchezeshaji uwanjani.
Kocha Maresca alisema Palmer alipata maumivu hayo tangu kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace wikiendi iliyopita.
Wakati wakiamini angecheza mechi ya West Ham, kiungo Palmer alishindwa kufanya hivyo na kuishia kukaa kwenye benchi.
Maresca alisema: "Cole kwa siku nne au tano zilizopita hakuwa fiti kwa asilimia 100. Alijaribu kufanya mazoezi ya kupasha misuli, lakini alihisi maumivu. Tumeona tusimuumize zaidi."
Palmer sasa atakuwa na muda zaidi wa kupona maumivu yake kwani Chelsea mchezo wao ujao utakuwa Agosti 30 itakapokipiga na Fulham. Hiyo itakuwa mechi pekee ya kiushindani ya Chelsea kati ya sasa na Septemba 13, hivyo Palmer atakuwa na muda wa kutosha wa kupumzika na kupona majeraha yake.