Alonso apewa Man City, Zidane, Klopp watajwa Real Madrid
Muktasari:
- Katika mechi saba zilizopita hivi karibuni za mashindano, Madrid imeshinda mechi mbili pekee, ikitoka sare tatu na kupoteza mbili.
Madrid, Hispania. Kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso, yuko kwenye wakati mgumu ndani ya kikosi hicho huku ripoti kutoka Hispania zikidai kuwa anaweza kupoteza ajira yake wiki hii endapo timu yake haitapata matokeo chanya dhidi ya Manchester City katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hali ya mambo imezidi kuwa mbaya kwa upande wa Madrid baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Celta Vigo juzi Jumapili, matokeo yaliyowaacha pointi nne nyuma ya vinara Barcelona mwezi mmoja tu baada ya kuwa mbele kwa pointi tano.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, ulitawaliwa na vurugu kufuatia wachezaji wawili wa Madrid kutolewa kwa kadi nyekundu, tukio ambalo limeongeza moto katika taarifa za kuwepo kwa mgawanyiko kati ya Alonso na baadhi ya wachezaji wake wakiwemo Jude Bellingham, Kylian Mbappe na Vinicius Jr.
Kikao cha dharura Bernabéu
Gazeti la Marca limeripoti kuwa Rais wa klabu, Florentino Pérez, aliitisha kikao cha dharura usiku wa Jumapili kujadili mwenendo mbaya wa timu, wingi wa majeruhi akiwemo beki Éder Militão anayetarajiwa kukaa nje kwa wiki kadhaa pamoja na malalamiko kuhusu ubora wa uchezeshaji wa marefa.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, uamuzi uliotolewa katika kikao hicho ni kwamba Alonso, aliyeanza kazi msimu huu akitokea Bayer Leverkusen, amebakiwa na siku chache kuokoa kibarua chake.
Hatima yake inadaiwa kutegemea pakubwa na matokeo ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Manchester City utakaopigwa kesho Jumatano, Desemba 10, 2025 kwenye dimba la Santiago Bernabeu.
Hadi sasa, Madrid inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa makundi ya Ligi ya Mabingwa ikiwa imepata ushindi katika michezo minne na kipigo kimoja kilichotolewa na Liverpool.
Katika mashindano yote, Madrid imeshinda mechi tatu pekee kati ya saba zilizopita, kiwango kilichoonekana kuwa chini ya matarajio ya mabosi wa klabu hiyo.
Zidane na Klopp waanza kutajwa
Inaelezwa kuwa tayari Madrid imeanza kuangalia mbadala wa Alonso endapo mambo yataendelea kuwa mabaya. Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Zinedine Zidane, ametajwa kama mmoja wa wanaoweza kurejeshwa, huku jina la Jurgen Klopp likitajwa kama pendekezo jingine.
Klopp aliachia ngazi Liverpool mwishoni mwa msimu wa 2023/24 kutokana na kuchoka na presha ya kazi, na kwa sasa anafanya kazi ndani ya kampuni ya Red Bull kama Mkuu wa Masuala ya Soka Duniani. Ingawa amewahi kusema hatarudi kwenye ukocha, Madrid imeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.
Zidane, aliyeipa Madrid kombe la Ligi ya Mabingwa mara tatu mfululizo, hajaiongoza timu yoyote tangu alipoondoka kwa mara ya pili mwaka 2021.
Taarifa kutoka Mundo Deportivo zinaeleza kuwa baadhi ya wachezaji hawajapendezwa na mtindo wa uongozi wa Alonso, ambaye anadaiwa kuwa na kauli kali tofauti na watangulizi wake akina Zidane na Carlo Ancelotti.
Wachezaji wanaodaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na kocha huyo ni pamoja na Vinicius Jr, Fede Valverde, Brahim Diaz, Rodrygo, Endrick na Ferland Mendy.
Valverde ameripotiwa kulazimika kucheza nje ya nafasi yake ya kiungo, akitumika mara kwa mara kama beki wa kulia wakati Dani Carvajal na Trent Alexander-Arnold wakisumbuliwa na majeraha. Diaz na Rodrygo pia wamekuwa wakitumika mara chache na mara nyingi kama wachezaji wa akiba.
Kijana wa Kibrazil, Endrick, amechezeshwa mechi moja tu msimu mzima baada ya kushindwa kumvutia kocha.
Kisa cha Vinicius Jr chachochea moto
Vinicius Jr ndiye mchezaji anayehusishwa zaidi na mgogoro na kocha wake. Katika El Clasico ya mwezi uliopita, alisikika akilalamika kwa hasira wakati akitolewa nje, akisema: “Ninaondoka kwenye timu hii.”
Hata alipoomba radhi baadaye kwenye mitandao ya kijamii, alijizuia kutaja jina la Alonso, jambo lililoibua maswali kuhusu uhusiano wao.
Taarifa zaidi zinadai kuwa mchezaji huyo hana mpango wa kuongeza mkataba wake unaomalizika mwaka 2027 endapo mazingira ya sasa yataendelea kuwa mabaya Bernabeu.