Amorim na mzigo mpya Man United, kitawaka
Muktasari:
- Kocha huyo mwenye umri wa miaka 39 ataanza kazi rasmi huko Old Trafford, Novemba 11, akikabiliwa na kibarua kizito cha kuipandisha timu hiyo kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuwa kwenye timu 10 za chini.
Kuna saa chache za kungoja kabla ya Ruben Amorim hajaanza rasmi kibarua chake huko Manchester United mahali ambako atakuwa na shughuli pevu kama anataka kukirejesha kikosi hicho kwenye makali ya kutamba kwenye michuano mbalimbali.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 39 ataanza kazi rasmi huko Old Trafford, Novemba 11, akikabiliwa na kibarua kizito cha kuipandisha timu hiyo kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuwa kwenye timu 10 za chini.
Amorim anatazamwa kama mmoja wa makocha wenye vipaji vikubwa Ulaya kwa sasa, lakini anakwenda kurithi kikosi chenye mapengo makubwa kwenye baadhi ya maeneo licha ya kutumia zaidi ya Pauni 200 milioni kwenye dirisha la usajili lililopita la majira ya kiangazi.
Tayari kumekuwa na uvumi Amorim anaweza kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Sporting Lisbon kunasa baadhi ya mastaa wa timu hiyo, akiwamo straika Viktor Gyokeres, ambaye ameonyesha uwanjani mchango mkubwa kutokana na kasi yake ya kutikisa nyavu.
Hata hivyo, Amorim amesisitiza hatarejea kwenye klabu yake hiyo ya zamani kusajili mastaa kwenye durisha la Januari, hata kama ni kwa Gyokeres, akimzungumzia staa huyo wa Sweden “atagharimu Euro 100 milioni”.
Atahitaji kufanya maboresho kwenye safu ya ulinzi, hasa kwa beki wa kati licha ya usajili wa Leny Yoro, ambaye bado hajaanza kuitumikia Man United msimu huu kutokana na kuumia kwenye pre-season na ilimsajili pia Matthijs de Ligt.
Beki wa kati, Jarrad Branthwaite anaweza kuwa chaguo sahihi kuboresha safu ya mabeki ya Amorim, hasa baada ya kocha Sean Dyche kukiri kwamba Everton inaweza kufungua milango ya kumpiga bei beki huyo, kwasababu timu hiyo inahitaji pesa.
Branthwaite ameshindwa kucheza msimu huu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na aliwekwa benchi kwenye mechi mbili za mwisho, hivyo dau lake linaweza kushuka na kuishawishi miamba ya Old Trafford kwenda kunasa saini yake, baada ya ofa zao mbili za Pauni 70 milioni kugomewa huko nyuma. Amorim anapenda kucheza na mabeki watatu, hivyo Branthwaite akinaswa atakwenda kucheza sambamba na De Ligt na Lisandro Martinez.
Beki mwingine anayehusishwa na Man United ni wa kushoto wa Bayern Munich, Alphonso Davies. Staa huyo wa kimataifa wa Canada kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na Mashetani Wekundu na wanafuatilia kila kitu kuhusu hatima yake.
Mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na kinachoelezwa ni kwamba Man United wanaweza kupelekea ofa Bayern wakati dirisha la Januari litakapofunguliwa. Davies ameendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Bayern akianzishwa kwenye mechi saba za Bundesliga msimu huu kutokana na Luke Shaw na Tyrell Malacia kuumia mara kwa mara, hivyo Amorim anaweza kwenda kumnasa Davies.
Man United itahitaji pia mchezaji wa kuwafungilia mabao, ambapo kwa sasa kinara wa mabao kwenye kikosi chao ni Alejandro Garnacho mwenye mabao sita, hivyo Amorim bila shaka atahitaji kuleta mtu kwenye eneo hilo la kufunga.
Klabu hiyo imekuwa ikihusishwa pia na Leroy Sane ambaye ni kama Davies mkataba wake huko Bayern Munich utakwisha mwisho wa msimu.
Amorim anaweza kufanya jaribio la kumsajili kwenye dirisha lijalo akienda kuwajaribu Bayern kwa ajili ya huduma ya staa huyo wa zamani wa Manchester City ambaye anaweza kumpata kwa dau la chini.
Sane hakuwa ameanza mechi yoyote ya Bundesliga chini ya Vincent Kompany msimu huu, ambapo alitokea benchi kwenye mechi tano, lakini amefanikiwa kufunga mabao matatu katika michuano yote. Amorim chaguo ni lake, kusubiri hadi mwisho wa msimu kumnasa bure au amchukue Januari kwenda kuimarisha kikosi chake na kukifanya kikosi kuwa na ushindani ndani ya uwanja.
Mchezaji wa nne ambaye Man United imekuwa ikihusishwa naye ni staa wa Sporting Lisbon, Geovany Quenda umri wake ni miaka 17 tu, lakini tayari klabu nyingi zinaanza kumfuatilia baada ya kung’ara kwenye ushindi wa 4-1 dhidi ya Man City, ambapo alicheza kwa dakika 85 na kutoa asisti. Ripoti zinafichua kwamba Man United inamtaka winga huyo, lakini anaweza kuwagharimu hadi Pauni 84 milioni na kuongeza idadi zaidi ya mastaa wa zamani wa Sporting kwenda kukipiga Old Trafford baada ya Cristiano Ronaldo, Nani na Bruno Fernandes.
Kikosi cha Kwanza cha Man United kinachotarajiwa: Onana; De Ligt, Martinez, Branthwaite; Dalot, Fernandes, Mainoo, Davies; Sane, Garnacho, Hojlund.