Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Amos Kabobo: kocha anayemudu michezo mingi

Amos Kabobo mzalishaji wa vipaji vya mchezo kikapu. Picha na Maktaba

Dar es Salaam. Katika umri wa miaka 30, Amos Kabobo 'Coach KB' angeweza kuwa mchezaji mahiri wa mpira wa kikapu lakini yeye ameamua kuwa mzalishaji wa vipaji vya mchezo huo kwa kujikita na ukocha.

Kwa sasa ni mwalimu wa michezo wa Shule ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DIS) iliyopo Masaki, Dar es Salaam lakini akifundisha michezo tofauti hasa mpira wa kikapu.

Hata hivyo, Kabobo hajawa mwalimu wa michezo wa shule hiyo kwa bahati mbaya na amefichua kwamba anafahamu vyema kucheza na kufundisha zaidi ya michezo 11 ambayo ni mpira wa kikapu, mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa pete, Tenisi, tenisi ya meza, Badminton, riadha, Cricket, kuogelea na michezo ya jadi.


Ukocha katika umri mdogo

Kabobo amefichua kwamba kutopata kocha mzuri wa kumfundisha kikapu wakati wa likizo na kukosekana kwa miundombinu mizuri kulichangia ageukia ukocha badala ya kucheza katika umri mdogo alionao.

"Niliona nisomee ukocha ili niweze kutimiza ndoto za wachezaji ambao hawana usimamizi na hawajui chaguo zipi wazifuate na kikubwa zaidi nilitamani kuwafundisha wachezaji ambao hawajui kabisa mchezo wa kikapu.

Kama mimi ambavyo sikuwa naujua mchezo huwo yaani kuwafundisha kuanzia sifuri hadi wawe mashujaa na kuwapa maarifa yote niliyonayo juu ya mchezo wa kikapu," anasema Kabobo.


Shule ipo kichwani

Kabobo ni mmiliki wa Shahada ya Kwanza ya Elimu ya Sayansi ya Michezo na Fizikia aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Elimu yake ya Sekondari aliipata katika Shule ya Vipaji Maalum ya Mpwapwa na elimu ya juu akapatia Shule ya Sekondari Kibiti.


Siri ya kupenda kikapu

Kabobo anasema kuwa alivutiwa na mmoja wa wachezaji wa mchezo huo walipokuwa shuleni hadi akaamua kujikita nao.

"Nilipenda kikapu kwa sababu nilivutiwa na na mmoja wa wachezaji ambao nilikutana nao Umisseta taifa akitokea mkoa wa Pwani alifahamika kwa jina la Mabangi ambaye kwa sasa ni mwanajeshi. 

"Alinivutia aina ya uchezaji wake na nikajikuta natamani kuujua mchezo huo na niliupenda na nikaujua kuucheza lakini sikubahatika kucheza kwenye ngazi za vilabu kutokana na ratiba za masomo na majeraha ya bega," alisema Kabobo.

Safari ya kimichezo ya Kabobo ilianzia 2013 alipoiwakilisha Kanda ya Kati katika michezo ya Umisseta akicheza mpira wa wavu na kutokana na uhitaji wa wachezaji wanaocheza zaidi ya mchezo mmoja, alilazimika kujifunza mpira wa kikapu na wa miguu.

Baada ya kuingia Chuo Kikuu alishiriki mashindano ya Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) na baadaye akasoma kozi mbalimbali fupi za ukocha.

Baada ya hapo akafanya kazi ya kufundisha kikapu katika taasisi ya SOS na shule za Hodari, Ahmes na DIA.


Ushauri kwa serikali

Ili kusaidia mchezo wa mpira kikapu kupiga hatua zaidi, Kocha Kabobo anaishauri serikali kuwekeza kwa watoto mashuleni, kujenga na kuboresha viwanja vya mchezo huo, mafunzo kwa makocha, kuongeza udhamini, kuandaa idadi kubwa ya mashindano na kuutangaza zaidi mchezo huo.