Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arsenal ilivyoivua Barcelona Ubingwa wa UEFA

Muktasari:

  • Arsenal imeivua Barcelona Ubingwa huo huku yenyewe ikifikisha mataji mawili.

Lisbon, Ureno. Timu ya wanawake ya Arsenal imeandika historia mpya baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa kwa wanawake Ulaya ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya bingwa mtetezi, Barcelona katika fainali iliyochezwa jana Mei 24 kwenye Uwanja wa José Alvalade, Lisbon,Ureno.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji Stina Blackstenius dakika ya 74, akiingia kama mchezaji wa akiba katika dakika ya 67.

Bao hilo lilitokana na kona iliyopigwa na Beth Mead, ambapo Blackstenius alitumia vyema nafasi hiyo kuipatia Arsenal ushindi ambao umewafanya kuwa mabingwa.

Safari ya Arsenal kuelekea Ubingwa

Arsenal ilianza kampeni yake ya msimu huu kwa ushindi wa 6-0 dhidi ya Rangers Septemba 4, 2024, kabla ya kuendelea na ushindi wa 1-0 dhidi ya Rosenborg katika raundi ya kwanza.

Katika raundi ya pili, walipoteza mchezo wa kwanza 1-0 dhidi ya BK Häcken lakini walirejea kwa kishindo kwa ushindi wa 4-0 katika mchezo wa marudiano na hivyo kufuzu hatua ya makundi.

Katika hatua ya robo fainali, Arsenal walikumbana na Real Madrid, ambapo walipoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 2-0 ugenini lakini walifanikiwa kushinda mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano walipokuwa kwenye uwanja wa nyumbani, na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.

Katika hatua ya nusu fainali, walikumbana na Lyon, mabingwa mara nane wa michuano hii, ambapo walipoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 2-1 wakiwa nyumbani lakini walishinda 4-1 katika mchezo wa marudiano uliopigwa ugenini, ambapo walifuzu fainali kwa jumla ya mabao 5-3.

Kocha Renée Slegers katika historia

Kocha wa Arsenal, Renée Slegers mwenye miaka 36, ambaye alijiunga na timu hiyo Oktoba 2024 baada ya kuondoka kwa Jonas Eidevall, ameweka historia ya kuwa kocha wa kwanza wa kike mwenye umri mdogo zaidi kutwaa taji hilo.

Slegers, ambaye ni raia wa Uholanzi, aliwahi kuwa mchezaji wa Arsenal katika ngazi ya vijana kabla ya kuhamia vilabu vingine vya Ulaya. Alistaafu soka kutokana na majeraha na kuanza kazi ya ukocha, ambapo alifanikiwa kuiongoza Rosengård ya Sweden kabla ya kujiunga na Arsenal kama kocha msaidizi.

Barcelona yavuliwa ubingwa

Barcelona, ambao walikuwa mabingwa watetezi wa ligi hiyo ya wanawake wameshindwa kutimiza azma hiyo. Timu hiyo ilikuwa imefika fainali kwa mara ya tano mfululizo na walikuwa wakilenga kutwaa taji la tatu mfululizo baada ya kulichukua taji hilo mwaka 2023 na 2024.

Rekodi kwa Arsenal

Ushindi huu unakuwa wa pili kwa Arsenal katika historia yao ya Ligi hiyo ya wanawake ya Mabingwa Ulaya, baada ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2007. Kwa upande wa Barcelona, wamefanikiwa kutwaa taji hili mara tatu, mwaka 2021, 2023, na 2024.

Katika mchezo huo, beki Leah Williamson alionesha kiwango cha juu hivyo kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo. Williamson, ambaye alirejea uwanjani baada ya kupona majeraha ya muda mrefu, alionesha kiwango bora na uwezo mkubwa katika safu ya ulinzi ya Arsenal.