Arsenal, Man United ngoma ya wakubwa
London, England. Arsenal leo inaikaribisha Manchester United kwenye Uwanja wa Emirates katika mchezo wa Ligi Kuu England (EPL) ambao kila upande utahitaji ushindi wa kuendeleza utawala dhidi ya mwenzake.
Kwa Arsenal, kupata ushindi katika mechi hiyo itakayoanza saa 1:30 usiku kwa muda wa Tanzania, kutaendeleza ubabe wake kwa Man United kwenye EPL ambapo itafikisha mchezo wa saba mfululizo bila kupoteza dhidi ya wapinzani wao hao.
Katika mechi sita zilizopita za Ligi Kuu England baina ya timu hizo, Arsenal imeibuka na ushindi mara tano na zimetoka sare mara moja.
Ushindi kwa Manchester United utaendeleza rekodi yao ya jumla ya ubabe dhidi ya Arsenal ambapo katika mechi 67 walizowahi kukutana, imepata ushindi mara 26, zimetoka sare mara 19 na Arsenal imeibuka na ushindi katika michezo 22.
Timu hizo zinakutana zikiwa zimetoka kupata matokeo yasiyopishana sana katika mechi zao tano zilizopita za EPL.
Wenyeji Arsenal katika mechi tano za Ligi Kuu England kabla ya mchezo wa leo, imeibuka na ushindi mara tatu na kutoka sare mbili huku ikipachika mabao nane na yenyewe imefungwa mabao matano.
Wageni Manchester United katika mechi tano zilizopita za EPL, wameibuka na ushindi mara mbili na wametoka sare tatu huku wakifunga mabao saba na wenyewe wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne.
Kuondoka na pointi tatu leo kutaifanya Arsenal izidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa EPL ambapo itafikisha pointi 53 na kwa upande wa Manchester United, ikipata ushindi leo itafikisha pointi 38.
Mchezo huo wa leo utachezeshwa na refa Craig Pawson atakayesaidiwa na Lee Betts. A Matt Wilkes huku refa wa akiba akiwa ni Thomas Bramall.
Ukiondoa mechi hiyo, kutakuwa na michezo mingine mitatu ya Ligi hiyo ambayo itachezwa katika viwanja na miji tofauti England leo.
Brentford itakuwa nyumbani katika Uwanja wa Brentford Community kuikaribisha Nottingham Forest na Crystal Palace itaialika Chelsea katika Uwanja wa Selhurst Park na katika Uwanja wa St. James’ Park, Newcastle United itakuwa mwenyeji wa Aston Villa.
Kesho kutakuwa na mchezo mmoja wa EPL ambao utazikutanisha Everton na Leeds United.