Man United yaporomoka klabu tajiri duniani
Muktasari:
- Hata hivyo, mapato ya kibiashara yanatarajiwa kubaki imara, baada ya klabu hiyo kupata pauni 346 milioni ikionyesha mvuto wao mkubwa duniani.
Manchester United imeshuka kutoka tano bora kwenye orodha ya klabu tajiri zaidi duniani, kufuatia kushindwa kuwa kwenye michuano ya Ulaya likiwa ni pigo lingine kwa utawala wa Ineos.
Kwa kipindi cha miaka 29, ambacho kampuni ya Deloitte imekuwa ikitoa orodha yake ya kila mwaka ya Football Money League, Manchester United imekuwa miongoni mwa klabu tajiri zaidi duniani.
Hata hivyo, baada ya kipindi kigumu uwanjani chini ya aliyekuwa kocha Ruben Amorim, United sasa inashika nafasi ya nane mwaka huu, ikiachwa kwa zaidi ya pauni 300 milioni na vinara Real Madrid.
Mabingwa hao wa Hispania wameongoza kwa mapato kwa msimu wa pili mfululizo, baada ya msimu uliopita kuandika historia kwa kuwa klabu ya kwanza kuvuka mapato ya euro 1 bilioni (sawa shilingi 2.9 trilioni).
Ripoti ya mwaka huu inaonyesha Real Madrid ikiongoza kwa mapato makubwa ya pauni 1.01 bilioni, huku mapato ya Manchester United ya pauni 692 milioni yakionekana madogo kwa kulinganisha na kipindi cha nyuma.
Hata hivyo, Real Madrid wana gharama kubwa zaidi za mishahara, wakitumia pauni milioni 446 kwa mishahara ya wachezaji, ikilinganishwa na pauni 353 milioni za Manchester United.
Manchester United pia wanakabiliwa na changamoto zaidi kuelekea ripoti ya mwaka ujao, kwani mapato yao ya siku za mechi ya pauni 166 milioni, yanatarajiwa kupungua kutokana na kutolewa mapema kwenye mashindano ya ndani na kukosa michezo ya Ulaya msimu huu.
Hata hivyo, mapato ya kibiashara yanatarajiwa kubaki imara, baada ya klabu hiyo kupata pauni 346 milioni ikionyesha mvuto wao mkubwa duniani.
Mtaalamu wa Deloitte, Tim Bridge, alisema hali ngumu ya United si ya kudumu.
“Ukirejea miaka 10 au 15 iliyopita, mapato ya siku za mechi ya Manchester United yalikuwa mfano kwa sekta nzima,” alisema.
“Uwezo wao wa kuzalisha mapato ya kibiashara ulikuwa kipimo cha klabu nyingine. Ingawa hali si ile ile sasa, fursa bado ipo.”
Aliongeza kuwa Manchester United bado ni moja ya chapa kubwa zaidi za soka duniani, lakini ili kufanikisha hilo kikamilifu, wanahitaji miundombinu bora na mbinu mpya za kushirikiana na mashabiki.
Klabu sita za Ligi Kuu England zimeingia kumi bora, huku Liverpool ikiongoza klabu za England baada ya kupata pauni 729 milioni kutokana na msimu wao wa kutwaa ubingwa wa Premier League. Manchester United wameshuka nafasi nne kutoka ya nne, wakibaki mbele ya Tottenham Hotspur na Chelsea pekee.
Manchester City, wapinzani wao wa jiji moja, walipata mapato ya pauni 723 milioni, huku Liverpool wakiwa na bili kubwa zaidi ya mishahara Englandpauni 437 milioni.
Katika ngazi ya Ulaya, Real Madrid, Barcelona na Paris Saint-Germain walitumia pesa nyingi zaidi kwa mishahara ya wachezaji. PSG waliongoza kwa mbali, wakitumia pauni 475 milioni zaidi ya nusu ya mapato yao yote ya pauni 730 milioni.
Chelsea wanashika nafasi ya 10, lakini takwimu zao zinaibua wasiwasi. Walipata pauni 90 milioni pekee kutoka mapato ya siku za mechi, hali inayoonyesha haja kubwa ya kuboresha uwanja wao wa Stamford Bridge wenye uwezo mdogo.
Pia walikuwa nyuma kibiashara, wakipata pauni 209 milioni , hali inayochangiwa na kukosa mdhamini wa jezi kwa muda mrefu.
Klabu tajiri zaidi duniani
Real Madrid
Barcelona
Bayern Munich
Paris Saint-Germain
Liverpool
Manchester City
Arsenal
Manchester United
Tottenham Hotspur
Chelsea