Man United yaipunguza kasi Man City mbio za ubingwa EPL
Muktasari:
- Man United imekusanya idadi ya pointi 35 katika michezo 22 ya Ligi Kuu England (EPL) huku Man City ikiwa imekusanya pointi 43 ikiwa nafasi ya pilk kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Manchester United imeivuta shati Man City katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) baada ya kuichapa kwa mabao 2-0 katika mechi baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford, Manchester England.
Mabao mawili ya Bryan Mbeumo na Patrick Dorgu yameifanya Man United kupata ushindi huo ambao umeigandisha Man City katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ambapo imebaki na pointi zake 43.
Manchester United yenyewe imepanda hadi ktika nafasi ya nne kwenye msimamo wa EPL ikifikisha pointi 35.
Kwa Man City, siku ya leo inaweza kuwa mbaya zaidi kwao ikiwa Arsenal itapata ushindi katika mchezo wa baadaye saa 2:30 usiku dhidi ya Nottingham Forest kwani itawatangulia kwa pointi tisa.
Imekuwa ni faraja zaidi kwa Meneja wa muda wa Man United, Michael Carrick ambaye ushindi wa leo umekuwa mwanzo mzuri kwake huku akijiandaa kuikabili Arsenal katika mechi inayofuata ya Ligi Kuu.
Mfungaji wa bao la kwanza la Man United, Mbeumo amesema kuwa ushindi huo ni matokeo ya sapoti kubwa waliyopata kutoka kwa mashabiki wao.
“Kufunga mbele ya jukwaa hili ni jambo nisiloamini. Katika mechi ya watani tena ndio zaidi. Tulitumia nishati ya mashabiki leo. Niliporejea vitu vingi vimebadilika.
“Lakini tuna kundi zuri sana. Siku zote tumekuwa wamoja na tunasisimama pamoja. Tuna umoja wa hali ya juu,” amesema Mbeumo.