Ayoub, Phiri kuibadili Simba SC

Dar es Salaam. Simba huenda ikamtumia kipa mpya, Ayoub Lakred katika mchezo wa Jumamosi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, huku pia eneo la ushambuliaji likifikiriwa kuwa na ladha tofauti kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Zambia.

Ukiachana na Lakred, huenda kwenye kikosi cha Simba kitakachoanza dhidi ya Dynamos kukawa na mabadiliko mengine kutokana na uamuzi ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Kocha huyo raia wa Brazil huenda asiwaanzishe Said Ntibazonkiza ‘Saido’ na Clatous Chama, ambao wamechelewa kujiunga na wenzao baada ya kutumikia timu zao za taifa.

Simba inaondoka nchini leo kwenda Zambia kwa ajili ya mchezo huo wa kuwania kutinga makundi ya mashindano hayo makubwa kwa ngazi za klabu Afrika, ikipanga kuvuka hatua ya robo fainali iliyokwama mara tatu.

Lakred alisajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu Morocco, Far Rabat, lakini tangu atue Msimbazi hajacheza wala kukaa benchi kwenye mechi ya kimashindano kutokana na kuchelewa maandalizi ya msimu (pre season).

Kipa huyo aliyesajiliwa kuziba pengo la Aishi Manula aliyeumia mwishoni mwa msimu uliopita na kufanyiwa upasuaji wa nyonga, alikosa mechi mbili za kimashindano ilizocheza Simba, ambazo ni zile za Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji, Simba ikishinda zote.

Hata hivyo, wakati wa mechi hizo alikuwa kikosini akijifua na kupata uzoefu na kujenga maelewano bora na wachezaji wenzake na kwa mujibu wa kocha wa makipa, Dani Cadena, Lakred yuko tayari kwa mchezo na watu watarajie kumuona kikosini Zambia.

"Eneo la kipa ni nyeti sana, hauwezi kufanya mabadiliko bila ya tathimini ya kina. Lakred ni kipa mzuri na anafanya vizuri mazoezini, hapo mwanzo tulimpa muda ili azoee na kuelewana vyema na wenzake, lakini kwa sasa yupo tayari kwa mchezo na ataonekana uwanjani," alisema Cadena.

Hata hivyo, katika mechi tatu za kirafiki za Simba dhidi ya Kipanga, Coasmopolitan na Ngome, Lakred amekuwa akidaka kwa kusaidiana na Ally Salim, Hussein Abel na Ahmed Feruz na kuonyesha kiwango bora, jambo linalomfanya Cadena kupanga kumpa nafasi kwenye mechi dhidi ya Dynamos.