Azam FC yamgeukia Kakolanya

MABOSI wa Azam FC wamegonga hodi Msimbazi wakimtaka kipa namba mbili wa timu hiyo, Beno Kakolanya, ikiwa ni siku chache tangu kuwepo kwa kelele za Mcomoro, Ali Ahamada anayelalamikiwa kwa kufungwa mabao ya kushangaza hasa yale ya mashuti ya mbali.

Ahamada ni kipa chaguo la kwanza Azam, lakini kiwango chake kimezua maswali mengi na kuwafanya mabosi wa timu hiyo ya Chamazi waanze harakati za kusaka kipa mwenye kiwango cha juu na jina la kwanza ni la Kakolanya anayesugua benchi kwa Aishi Manula pale Msimbazi.

Mwanachi imepenyezewa taarifa kwamba, mmoja wa mabosi wa juu wa Azam ameulizia mkataba wa Kakolanya na alipoambiwa umebaki miezi sita ametaka wamuombe kwa mkopo au kuuvunja.

“Bosi mmoja wa Azam baada ya kupoteza mechi yao na Yanga alimtafuta Kakolanya na kumwambia wanamuhitaji sana kwa sasa na walitaka kujua utayari wake lakini yeye aliwaambia ana mkataba lakini kigogo huyo alisema sio ishu,” kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti linafahamu Azam imeomba kwa Kakolanya kujua tarehe rasmi ya kumalizika kwa mkataba wake wa miezi sita ili kuangalia namna ya kuuvunja na kumlipa mara mbili ya mshahara anaolipwa Msimbazi endapo itamsajili.

Kaimu Msemaji wa Azam FC, Hasheem Ibwe alisema: “Kweli tuna mipango ya kusajili kipa kwa ajili ya kuja kusaidiana na waliopo ila kwa sasa niseme sina taarifa za kuwepo kwa mazungumzo yoyote na Kakolanya.”