Azam yatinga fainali ASFC baada ya miaka minne

Muktasari:

  • Hii ilikuwa nusu fainali ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kutokana na ubora wa timu zote ambao wamekuwa wakiuonyesha kwenye Ligi Kuu msimu huu.

AZAM FC leo ilitangulia kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), baada ya kuichapa Simba mabao 2-1 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara.

Hii ilikuwa nusu fainali ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kutokana na ubora wa timu zote ambao wamekuwa wakiuonyesha kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Azam ndiyo walikuwa wa kwanza kupachika bao kupitia kwa beki wao wa kulia Lusajo Mwaikenda, akimalizia mpira uliotemwa na kipa Ally Salim na kuipa timu yake bao la kuongoza lakini dakika ya 28 Simba walisawazisha kupitia kwa Sadio Kanoute ambaye alifunga bao safi kwa kichwa kutokana na   mpira wa adhabu uliopigwa na Said Ntibazonkiza'Saido' na kuzipeleka timu hizo mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Mshambuliaji wa Azam, Prince Dube ambaye aliingia kipindi cha pili ndiye aliyewaua Simba baada ya kufunga bao safi la pili kwenye mchezo huo katika dakika ya 74, zikiwa ni dakika tano tu tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Idris Mbombo.

Hili ni bao la tatu Dube anawafunga Simba msimu huu baada ya kuwafunga kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu Bara, ule wa sare ya bao 1-1 na ule wa pili ambao Azam walipata ushindi wa bao 1-0.

Wachezaji wa Azam walioanza ni:
Idrissu Abdullai,Lusajo Mwaikenda,Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Daniel Amoah,Issa Ndala, Sospeter Bajana,Ayoub Lyanga/Nathaniel Chilambo,James Akaminko, Idris Mbombo/Prince Dube,  Abdallah Sopu.
Simba walianza:

Ally Salim, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Joash Onyango, Henock Inonga, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Kibu Denis/Pape Sakho, Said Ntibazonkiza'Saido', Jean Baleke/John Bocco, Clatous Chama.