Baada ya Azam Complex sasa ni Amaan
Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya soka nchin, timu nne za Tanzania zimefuzu kwa hatua ya makundi ya mashindano ya CAF.
Yanga na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa na Azam FC na Singida Black Stars kwenye Kombe la Shirikisho.
MAAJABU YA AZAM COMPLEX
Azam FC na Singida Black Stars walifuzu wakiutumia uwanja wa Azam Complex.
Hii ikamaanisha kwanza hizi zinakuwa timu za tano na sita mtawalia kufuzu hatua ya makundi kupitia uwanja huo; baada ya Namungo 2021, Yanga 2022 na 2023 Simba 2023 na Stade Malien ya Mali mwaka 2023.
Naam, Stade Malien ya Mali, ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2023 kwa kuwatoa Aigle Noir Makamba FC ya Burundi.
Warundi ndio waliutumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani.
Timu hizi sita zinaufanya uwanja huo kuweka rekodi ya Afrika kwa kuzibeba timu nyingi zaidi kufikia makundi.
Huu ni muendelezo wa umuhimu wa uwanja huo kwenye soka, ndani na nje ya nchi yetu.
Mwaka 2024, uwanja huu ulikuwa 'bize' kwa kushuhudia mechi za CAF kwa siku tatu mfululizo.
Ilikuwa wikendi moja ya Agosti 16 hqdi 18 mwaka 2024.
Ijumaa ya Agosti 16 kulikuwa na mechi mbili; moja ya ligi ya mabingwa na nyingine ya Shirikisho.
Altar Solar ya Djibout ilianza na Dekedaha FC ya Somalia, saa kumi alasiri, kisha saa tatu usiku ikaja mechi ya Horseed ya Somalia na Rukinza FC ya Burundi.
Jumamosi Agosti 17 Vital'O ya Burundi iliikaribisha Yanga ya Tanzania.
Na Jumapili ya Agosti 18, Azam FC walicheza na APR ya Rwanda.
Lakini kubwa kuliko zote ni hii hapa.
Septemba 16. 2021 Azam Complex iliikusanya Afrika kwa kushuhudia timu sita kutoka mataifa tofauti barani zikifanya mazoezi siku hiyo kujiandaa na mechi za CAF.
Azam FC na Biashara United kutoka Tanzania, Horsted kutoka Somalia, Dikhil FC (Djibouti), Le Mesenger de Ngozi (Burundi) na US Gendermarie (Niger).
Haya yalikuwa maajabu mengine ya uwanja huu.
MAAJABU YA NEW AMAAN COMPLEX
Timu tatu za bara; Azam FC, Singida Black Stars na Yanga SC, zimeuchagua uwanja wa New Amaan Complex kwa mechi za hatua ya makundi.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mechi za hatua hii kufanyika katika uwanja huo wa kihistoria.
Na pia itakuwa mara ya kwanza kwa timu tatu kutumia uwanja mmoja kwenye hatua hii ya mashindano ya CAF. Haya ni maajabu makubwa sana.
Lakini hata hivyo uwanja huu una maajabu yake makubwa zaidi ya haya. Huu ndio uwanja wa kwanza kuwa na taa, Afrika Mashariki.
Uwanja huu uliwekewa taa tangu ulipojengwa kwa mara ya kwanza na kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julius Nyerere. Mwaka 1971.
Mwaka 1975 mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) yalifanyika hapo na kushuhudia mechi za usiku, ikiwemo fainali ya Simba na Yanga.
Huu ndio uwanja ulioziunganisha TANU na ASP mwaka 1977 na kuzaliwa CCM.
Bendera za vyama hivi viwili vya kupigania uhuru zikapepea kwa mara ya mwisho uwanjani hapo kabla ya kushushwa na kupandishwa bendera ya CCM kwa mara ya kwanza.
Uwanja wa Amaan umeshudia nusu fainali mbili za vilabu kwenye mashindano ya CAF, hivyo kuupiku uwanja wa Mkapa, na kulingana na Uhuru.
Nusu fainali ya Malindi mwaka 1995 Kombe la CAF na Simba mwaka 2025 Kombe la Shirikisho, zinaufanya uwanja huo kuwa sawa na Uhuru kwa nusu fainali mbili, Simba 1974 Klabu Bingwa Afrika na Simba tena 1993 Kombe la CAF.
Mkapa imechezwa nusu fainali moja tu, ya Yanga 2022 Kombe la Shirikisho...zaidi ya hapo ni timu ya taifa. CHAN 2024.
Ukiutaja uwanja wa Mkapa unagusa moja kwa moja historia ya uwanja wa Aman ambao ulijengwa na wachina.
Huu ndio uwanja wa kwanza kujengwa ma watching barani Afrika, na ujenzi wake ukafungua milango ya wachina kujenga viwanja barani Afrika...hadi uwanja wa Mkapa.
Haya yote ni maajabu ya New Aman Complex.
Lakini juu ya yote haya. Uwanja wa New Amaan Complex, Azam Complex na Mkapa ambao upo kwenye kijiji changamani ambacho maana yake ya Complex pia, vina ukubwa sawa kwa eneo la kuchezea.
Viwanja hivi vina vipimo vya mita 105 urefu na mita 68 upana.
Hiki ndicho kipimo 'standard ' cha FIFA kwa viwanja vya mpira.
Tumeshaona maajabu ya Azam Complex kubeba timu nyingi kufuzu hatua ya makundi, sasa kusubiri kuona maajabu ya New Amaan Complex kuzibeba timu nyingi kufuzu robo fainali.
Inshallah inawezekana.
Mungu ibariki Tanzania