Bakhresa ajenga uwanja Qatar, aweka rekodi mpya

DOHA, QATAR. FAINALI za Kombe la Dunia zimefunguliwa rasmi juzi Jumapili kwa mchezo mmoja mwenyeji akianza Qatar dhidi ya Ecuador kwenye mechi ya ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia na kufungwa mabao 2-0.

Maandalizi ya viwanja vinane vitakavyotumiwa na mataifa 32 yanayoshiriki fainali hizi Qatar, yamegharimu mamilioni ya pesa hadi kukamilika. Jumla ya mechi 64 zitachezwa hadi Desemba 18 zitakapokamilika.

Mashabiki zaidi ya bilioni moja wameshangazwa na uzuri wa viwanja hivyo na mafanikio ya miundo mbinu hiyo kutokana na ubunifu uliotumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanja hivyo vinane. Viwanja vingine vitakavyotumika kwenye fainali hizo ni Ahmad Bin Ali, Al Janoub, Al Thumama, Education City, Khalifa International, Al Bayt na Stadium 974.

Mkandarasi anayetoka kwenye familia ya mfanyabiashara maarufu Tanzania, Said Salim Bakhressa, Saeed Abdullah Bakhressa, alikuwa miongoni wa wafanyakazi waliojenga Uwanja wa Lusail Stadium, utakaotumika kwa ajili ya mechi ya fainali za Kombe la Dunia. Mkandarasi huyo aliweka wazi tangu ujenzi huo ulipoanza na changamoto walizozipitia na kuweka historia ya kuipa Tanzania heshima kubwa kutokana na kazi ya mikono yake. Kwa mujibu wa Saeed mwenye nasaba na mfanyabiashara huyo maarufu nchini, amesema uwanja huo umejengwa chini ya Kampuni ya HBKCRCC ikishirikiana na Shirika la Ujenzi la Reli la China.


UJENZI ULIANZA LINI?

Saeed alisema ujenzi huo ulianza tangu mwaka 2017 akiwa kama meneja mpaka unakamilika mwaka huu kabla ya fainali za Kombe la Dunia. Mkandarasi huyo ndiye aliyekuwa akipanga kila kitu na kuwaongoza wafanyakazi wenzake. Alisamamia mambo mbalimbali ya ujenzi wa uwanja huo kama michoro na vipimo. Saeed alikuwa bega kwa bega na wafanyakazi kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa na hakuna kinachobadilika. Alisema:

“Tulianza mradi wa ujenzi huu tangu mwaka 2017, nilikuwa ndiye meneja na injinia wa ujenzi wa uwanja huu, nilikuwa nasimamia wafanyakazi wote waliohusika na ujenzi hadi ulipokamilika,” alisema mkandarasi huyo.

GHARAMA YA UJENZI

Ujenzi wa Uwanja wa Lusail umegharimu kitita cha 1.7 trilioni hadi ulipokamilika. Kwa mujibu wa mkandarasi huyo mechi 10 za Kombe la Dunia zitachezwa kwenye uwanja huo.

Argentina itatumia uwanja huo kwa mara ya kwanza itakapomenyana dhidi ya Saudi Arabia kesho Jumanne. Kitu ambacho Saeed anajivunia ni uwanja huo kukamilika kwa wakati.

Akizungumza baada ya kuweka rekodi hiyo, alisema: “Siku zote itabaki kwenye kumbukumbu zangu, najivunia kuwa sehemu ya ujenzi wa uwanja huu, umejengwa kwa viwango vya juu na utakuwa kumbukumbu ya Qatar na dunia nzima kwa ujumla,” alisema Saeed.


CHANGAMOTO WALIZOPATA

Licha ya kukamilisha kwa wakati, Saeed alisema walipitia changamoto na haikuwa rahisi hadi uwanja huo ulipokamilika kwa wakati. Wafanyakazi walipambana kuhakikisha mambo yanakwenda na kutatua makosa yaliyojitokeza wakati ujenzi huo ulipokuwa ukiendelea.

“Ubunifu wa uwanja huu ulichelewa kukamiliaka kwa hiyo tulilazimika kufanya mahesabu na kuanza ujenzi kabla ya usanifu kupitishwa. Hatua hiyo ndiyo iliyosababisha uwanja kukamilika kwa wakati hatukutaka kupoteza muda,” alisema Saeed.