Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baleke, Sawadogo ngoja tuone

SIMBA sasa inatamba mtaani baada ya kushusha watu wa kazi watatu kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Jumapili na wote hao watakuwepo kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati chama lao jipya litakapokuwa likicheza na Mbeya City mechi ya Ligi Kuu.
Mastaa wapya ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao ni mshambuliaji Jean Baleke akisajiliwa kwa mkopo wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwaka mwingine kutokea kwa miamba ya DR Congo, TP Mazembe, Kiungo mkabaji Mburkinafaso, fundi Ismael Sawadogo kutokea Difaa El Jadida aliyowahi kuichezea Mtanzania Simon Msuva na Mshambuliaji Said Ntibanzokiza 'Saido' ambaye tayari alianza kazi kikosini hapo kwa kutupia mabao matatu 'Hat trick', na kutoa asisti moja kwenye mechi yake ya kwanza Simba ikiichapa 7-1 Tanzania Prisons.
Saido tayari ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha Simba tangu ajiunge nao mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, Sawadogo naye yupo nchini na jana baada ya timu kuwasili ikitokea Dubai ilikoweka kambi maalumu alijiunga na wenzake na Baleke kufika leo jioni atakuwa tayari kambini na wenzake kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuwavaa Mbeya City kesho.
Baleke anayecheza eneo la mshambuliaji wa kati ametua Simba akitokea Nejmeh SC ya Lebanon alikokuwa kwa mkopo akitokea Mazembe na katika mechi 11 za mwisho alizocheza amefunga mabao matatu na kutoa asisiti moja lakini ikumbukwe kuwa aliwahi kuchukua kiatu cha mfungaji bora wa ligi ya DR Congo mwaka 2021, akiwa Mazembe na kumaliza na mabao 14 huku akifuatiwa na staa wa sasa wa Yanga Fiston Mayele aliyekuwa na 11 wakati huo akiichezea AS Vita Club.
Kwa upande wa Sawadogo ambaye nje ya kuwa bora kwa kukaba pia anasifika kwa ufundi wa kumiliki mpira na kupiga pasi, kabla ya kutua Simba alikuwa akipiga tizi la kufa mtu kwenye viwanja na gym tofauti baada ya kupona majeruhi na leo atakuwa uwanjani sambamba na kina Baleke na Saido hivyo ni uamuzi wa kocha mkuu wa Simba, Mbrazili Oliviera Roberto 'Robertinho' kuamua kuwatumia au kuwaacha washangae shangae kwanza mazingira ya kwa Mkapa na Dar kwa ujumla.


KIKOSI KIMETIMIA
Tangu alivyotua Robertinho Simba, alikiangalia kikosi na kusema anataka mshambuliaji wa kati na kiungo wa kazi haraka na mabosi wa chama hilo hawakufanya utani na kuwashusha Baleke na Sawadogo hivyo ni kama kikosi alichotaka kimetimia na sasa ni kazi kwake aamue timu ichezeje na kwa kuwatumia wachezaji gani.
Ongezeko la Baleke katika eneo la ushambuliaji litampa machaguo mengi kwani kabla yake walikuwa wakicheza Moses Phiri mwenye mabao 10 hadi sasa ambaye ameanza mazoezi mepesi baada ya kupona majeruhi aliyoyapata, John Bocco mwenye mabao tisa,  na Habib Kyombo mwenye mawili huku ingizo jipya, Saido na kiungo Clatous Chama nao wakinogesha eneo hilo.
Hivyo Robertinho ataamua amtumie, Baleke kama mshambuliaji wa kati namba 9 au 10 kwani anamudu kucheza kote huko na amekuwa mtaalamu wa kucheka na nyavu kutokana na kuwa na nguvu nyingi mguuni na jicho la goli.
Katika eneo la kiungo mshambuliaji na winga, Robertinho atachagua awatumie kina nani kati ya Chama, Phiri, Saido, Mzamiru au Pape Sakho ambao wote kwa sasa wako moto lakini pia ana machaguo mengine mengi wakiwemo Kibu Denis aliyemkubali mazoezini, Peter Banda, Agustine Okrah na Jimmyson Mwanuke.
Katika eneo la Sawadogo (Kiungo mkabaji), Robertinho sasa ana machaguo mengi na atachagua mwenyewe aanze na nani, kati ya Sawadogo, Mzamiru na Sadio Kanoute walio katika kiwango bora sasa, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, na kiraka Nassoro Kapama lakini pia anaweza kutumia viungo wawili wakabaji kutokana na aina tofauti za mifumo.
Hata hivyo, kocha Robertinho aliwashukuru viongozi wa Simba kwa kambi ya Dubai na usajili walioufanya na kuweka wazi kuwa kikosi sasa kipo tayari kwa mapambano.
"Angalau nimepata muda kiasi wa kukaa na timu na kucheza mechi za kirafiki ambazo zimenipa mwanga wapi pa kuanzia, ni jambo zuri na tunaushukuru uongozi. Nadhani kwa sasa tunaweza kuendelea na mapambano kwani timu imekamilika kutokana na usajili kumalizika na waliokuwa majeruhi wameanza kurejea," alisema Mbrazili huyo aliyetua Simba akitokea Vipers ya Uganda.