Barcelona yafunguka usajili Rashford
Muktasari:
- Rashford alifunga bao lake la kwanza wiki mbili zilizopita katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Newcastle United ugenini.
Mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco amesisitiza kwamba klabu hiyo imevutiwa sana na kiwango ambacho mshambuliaji wa kimataifa wa England, Marcus Rashford amekionyesha lakini haitokuwa na ulazima wa kumsainisha mkataba wa moja kwa moja ikiwa hawatohitaji kufanya hivyo ifikapo mwisho wa msimu huu.
Rashford ambaye amejiunga na Barca kwa mkopo wa msimu mmoja, hadi sasa ndiye mchezaji aliyehusika na mabao mengi zaidi klabuni hapo (sita) akifunga mawili na kutoa asisti nne ikiwemo moja ya Ligi ya Mabingwa jana dhidi ya PSG.
Akizungumza na gazeti la Mundo Deportivo la Hispania, Deco alisema: "Ni mapema mno kuzungumza uamuzi wa msimu ujao. Muhimu kwa sasa ni kwamba tunafurahishwa naye."
"Anatupa kile tulichotarajia. Ni mchezaji wa kiwango cha juu. Aling’ara akiwa na umri mdogo sana, kisha akawa na wakati mzuri sana akiwa na Man United ingawa baadae alipita nyakati ngumu na naelewa ni kwa sababu ya mabadiliko ya makocha na pia alikuwa akitegemewa sana, yote kwa yote sisi tunafurahishwa na anachokifanya katika timu yetu, uamuzi wa kumbakisha au kutombakisha siwezi kuujadili sasa, acha tuangalie mechi zinazofuata, uamuzi utafanyika tu."
Rashford alikuwa akiwindwa na Barcelona tangu Januari mwaka huu lakini ilishindikana mwishowe alijiunga na Aston Villa, ambapo alifunga mabao manne na kutoa asisti sita katika mechi 17 za michuano yote.
Baada ya msimu uliopita kumalizika, alijiunga na Barca katika dirisha lililopita na kwenda kuongeza nguvu katika safu yao ya ushambuliaji ambayo ina mastaa wengine kama Raphinha, Lamine Yamal, Ferran, Fermin Lopez na Robert Lewandowski.
Rashford alifunga bao lake la kwanza wiki mbili zilizopita katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Newcastle United ugenini.