Barcelona yavunja rekodi Kombe la Dunia
Muktasari:
- Barcelona imekuwa na uwakilishi mkubwa wa wachezaji katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia ambayo yenyewe ndio ilikuwa inaishikilia
Kitendo cha Hispania kuingia hatua ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka huu, kimeifanya klabu ya Barcelona kuvunja rekodi yake ya mwaka 2010.
Rekodi hiyo ni kuwa klabu ambayo imekuwa na uwakilishi mkubwa wa wachezaji katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia ambayo yenyewe ndio ilikuwa inaishikilia.
Kabla ya mechi ya jana baina ya Argentina na England, Barcelona ilikuwa na uhakika wa kuwa na wachezaji nane kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka huu itakayochezwa Julai 19 katika Uwanja wa MetLife.
Wachezaji hao wote wapo kwenye kikosi cha Hispania ambao ni Lamine Yamal, Pedri, Gavi, Pau Cubarsi, Eric Garcia, Dani Olmo, Ferran Torres na Joan Garcia.
Mwaka 2010, Barcelona ilikuwa na uwakilishi wa wachezaji saba katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi ambayo ilipata ushindi wa bao 1-0.
Wachezaji hao saba walikuwa ni Carles Puyol, Gerard Piqué, Sergio Busquets, Xavi Hernández, Andrés Iniesta, Pedro Rodríguez na David Villa.
Jana Hispania ilifanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ufaransa.
Mabao ya Hispania yalipachikwa na Mikel Oyarzabal na Pedro Porro.
Ushindi huo umeifanya Hispania irudi katika hatua ya fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16 tangu ilipofanya hivyo mwaka 2010 wakati mashindano hayo yalipofanyikia Afrika Kusini.