Bayer Leverkusen yaweka rekodi Ulaya
Muktasari:
- Kwa mara ya mwisho Leverkusen kuambulia kichapo ulikuwa mchezo wa mwisho wa msimu wa 2022-23, ilipolala kwa mabao 3-0 dhidi ya VfL Bochum.
Munich, Ujerumani. Bayer Leverkusen imeweka rekodi ya timu ambayo haijapoteza mechi nyingi barani Ulaya baada ya jana kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya AS Roma na kufikisha michezo 49.
Vijana hao wa kocha Xabi Alonso walionekana kuwa wanaelekea kupoteza mchezo huo baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-1 dhidi ya Roma hadi dakika ya 97 lakini walisawazisha kupitia kwa Josip Stanisic na kwenda kwenye fainali ya Kombe la Europa.
Awali Roma ilionekana inakwenda fainali baada ya hadi dakika ya 66 kuwa mbele kwa mabao 2-0, yote yakiwa yameweka kimiani na Leondro Paredes kwa mikwaju ya penalti.
Hata hivyo, Leverkusen ilifunga bao moja katika dakika ya 83 kupitia kwa Gianluga Mancini na kufunga la pili mwishoni lililomaliza ndoto ya Roma ya kwenda fainali.
Sare hiyo ambayo imewapa Leverkusen ushindi wa jumla wa mabao 3-2 imewafanya watinge fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Ulaya baada ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Sasa timu hiyo imefanikiwa kufuzu kwa fainali hiyo ambapo itavaana na Atalanta Mei 22 mwaka huu.
Kwa mara ya mwisho Leverkusen kuambulia kichapo ulikuwa mchezo wa mwisho wa msimu wa 2022-23, ilipolala kwa mabao 3-0 dhidi ya VfL Bochum.
Sasa timu hiyo inakaribia kutwaa makombe matatu kwa msimu mmoja, ikiwa imeshatwaa Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga ipo fainali ya DFB Pokal na fainali ya Europa itakayopigwa Dublin.
Akizungumza baada ya mchezo huo Alonso amesema anafurahi kwa kuwa timu yake imefunga dakika za mwisho kwenye michezo mingi, lakini anawapa tahadhari kuwa kuna siku bao la mwishoni litakosekana.
"Ni furaha kufunga bao hili mwishoni mwa mchezo, nafikiri baada ya sisi kufunga filimbi ilipulizwa kuwa mechi imemalizika, lakini tahadhari yangu ni kwamba kuna siku tutakosa bao la muda huu na tutapoteza mchezo muhimu.
"Awali tulikuwa na nafasi nyingi lakini tukashindwa kuzitumia, nafikiri siyo jambo zuri, lazima tujipange vizuri kwenye michezo ijayo," alisema kocha huyo.
Timu kumi ambazo zinashikilia rekodi ya kutopoteza Ulaya:
49 – Bayer Leverkusen (2023–)
48 – Benfica (1963–1965)
45 – Dinamo Zagreb (2014–2015)
45 – Rijeka (2016–2017)
44 – Rangers (1992–1993)
43 – Juventus (2011–2012)
42 – Milan (1991–1992)
42 – Ajax (1995–1996)
41 – The New Saints (2023–2024)
40 – Fiorentina (1955–1956).