Ugumu PSG, Dortmund uko hapa

Muktasari:

  • Mshindi wa mechi hiyo ataungana na yule atakayepenye baina ya Real Madrid na Bayern Munich kucheza fainali ambayo imepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Wembley, Juni Mosi.

Paris,Ufaransa. PSG inaikaribisha Borussia Dortmund leo katika Uwanja wa  Parc des Princes ikiwa na deni la kulipa ili isonge mbele na kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupoteza mechi ya kwanza wiki iliyopita kwa kichapo cha bao 1-0.

Katika mchezo wa leo, PSG itahitajika kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili iende fainali lakini kama itatoka sare au itapoteza maana yake itaaga mashindano hayo.

Wakati wenyeji PSG wakisaka fainali ya pili ya mashindano hayo baada ya kuingia kwa mara ya kwanza na ya mwisho msimu wa 2019/2020, Dortmund yenyewe ikipenya leo itakuwa inaingia hatua hiyo ya mwisho na ya juu zaidi katika mashindano ya klabu Ulaya kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo msimu wa 1996/1997 ilipochukua ubingwa na msimu wa 2012/2013 ilipoishia katika nafasi ya pili.

Wachezaji Lucas Hernandez, Presnel Kimpembe, Layvin Kurzawa na Sergio Rico watakosekana upande wa PSG leo kutokana na majeraha wakati Borussia Dortmund yenyewe itawakosa majeruhi Ramy Bensebaini na Julien Duranville huku Julian Ryerson na Sebastien Haller wakiwa kwenye hatihati.

Refa kutoka Italia, Daniele Orsato ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo akisaidiwa na wenzake kutoka nchi moja ambao ni Ciro Carbone na Alessandro Giallatini huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Davide Massa.

Marefa ambao watakuwa katika chumba cha teknolojia ya video ya usaidizi kwa waamuzi (VAR) nao wanatoka Italia ambao ni Massimiliano Irrati na Paolo Valeri.

Mshindi wa mechi hiyo ataungana na yule atakayepenye baina ya Real Madrid na Bayern Munich kucheza fainali ambayo imepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Wembley, Juni Mosi.

Pamoja na PSG kuwa nyumbani na Dortmund kushinda mchezo wa kwanza, mchezo wa leo unaonekana ni mgumu kutabirika kwa timu ipi inaweza kusonga mbele kutokana na sababu mbalimbali hivyo hapana shaka itakuwa ya ushindani wa aina yake.

Kuna sababu tatu ambazo zinafanya mechi ya leo kuonekana kuwa na ugumu kwa pande zote mbili ingawa timu moja inaingia na faida ya kucheza nyumbani na nyingine ina jeuri ya kuwa na ushindi wa mechi ya kwanza.


Matokeo yanayofanana

Timu hizo mbili katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti zimekuwa na matokeo yanayoshabihiana hivyo hazionekani kupishana sana katika muendelezo wa ubora.

Katika mechi tano zilizopita kabla ya kukutana leo, PSG na Borussia Dortmund kila moja imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare moja na zote zimepoteza mechi mojamoja.

Ushindi wa PSG ni dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na dhidi ya Lorient na Lyon kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa ambayo pia mchezo mmoja ilitoka sare na Le Havre huku ikipoteza na Dortmund kwenye mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa upande wa Borussia Dortmund, imepata ushindi kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid na PSG na kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, imapeta ushindi dhidi ya Augsburg, kutoka sare na Bayer Leverkusen na kupoteza mbele ya RB Leipzig.


Ukuta dhaifu

Timu hizo zinakabiliana huku zikiwa na takwimu zisizovutia katiak safu zao za ulinzi na hilo linajidhihirisha na kile ambacho zimefanya katika mechi tano zilizopita kwa kila moja.

Katika mechi hizo tano zilizopita za mashindano tofauti, PSG imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane ikiwa ni wastani wa bao 1.6 kwa mchezo.

Kwa upande wa Borussia Dortmund, haina tofauti sana na kile kilichofanywa na safu ya ulinzi ya PSG kwa kuruhusu mabao nane.


Maadui wa nyavu

Wakati safu zao za ulinzi zikionekana kuyumba, timu hizo zimeonekana kuwa moto wakuotea mbali katika kufunga mabao na zina wastani mzuri katika eneo hilo.

Wenyeji PSG katika michezo mitano iliyopita ya mashindano tofauti wamefunga mabao 15 ikiwa ni wastani wa mabao matatu kwa kila mchezo.

Borussia Dortmund wao katika mechi tano zilizopita, wamefunga mabao 12 ikiwa ni wastani wa mabao 2.4 kwa mechi.