Beckebauer afariki dunia
Muktasari:
- Gwiji zamani wa soka Franz Beckebauer amefariki dunia huku akiacha kumbukumbu ya kuingia kwenye kitabu cha wanasoka waliofanya vizuri ndani na nje ya uwanja.
Ujerumani. Familia ya Gwiji wa soka, Franz Beckebauer (78) imethibitisha kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Bayern Munich na Ujerumani amefariki dunia jana kutokana na udhaifu wa mwili uliosababishwa na magonjwa mbalimbali.
Kifo cha mchezaji huyo kimetangazwa leo ikiwa ni siku chache tangu dunia ilipoondokewa na gwiji mwingine wa soka, Mario Zagallo wa Brazil.
Beckenbauer anakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa wachezaji wachache walioshinda mataji yote makubwa duniani ya soka kwa ngazi ya klabu na timu za taifa.
Kwa nyakati tofauti ameshinda taji la Ligi Kuu ya Ujerumani 'Bundesliga', Kombe la Washindi Ulaya na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mataji hayo yote alishinda akiwa katika kikosi cha Bayern Munich aliyoitumikia kuanzia 1964 hadi 1977.
Alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu, kombe moja la Mabara, mataji manne ya Bundesliga, taji moja la washindi Ulaya na pia ana mataji manne ya DFB Pokal.
Akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani, Beckenbauer alifanikiwa kushinda Kombe la Dunia mwaka 1974 huku akishinda taji la Ulaya mwaka 1972.
Akiwa kocha, Beckenbauer aliiongoza Ujerumani kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1990.
Kiujumla, Beckenbauer alicheza jumla ya mechi 754 kwa ngazi ya klabu na kufunga mabao 98 huku akifunga mabao 14 katika mechi 103 za timu yake ya taifa.