Beki amvuta Fei Toto Simba kimtindo

BEKI wa pembeni wa zamani wa Simba, Said Sued ‘Panucci’ amesema ; “Anatumika Clatous Chama lakini asipokuwepo timu inayumba, sasa hilo ni tatizo ni tofauti na Yanga ina viungo wazuri wachezeshaji kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Salum Abubakary ‘Sure Boy’.”

Amewasisitiza viongozi wa klabu hiyo kuvunja benki na kufanya usajili katika maeneo matatu.

Sued aliyeichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa kama beki wa kulia aliiambia Mwanaspoti Simba sio kwamba ina kikosi kibaya msimu huu bali wachezaji wa timu hiyo hawajitumi kama ilivyo kwa wenzao Yanga.

Alisema Yanga ina wachezaji wazuri lakini jinsi wanavyojitolea uwanjani ndio sababu kubwa ya kuonekana hawashikiki tofauti na Simba ambayo inabebwa na wachezaji wachache mno.

“Yanga kuwa moto kwa sasa sio kwamba ni wazuri sana ila wachezaji wao wana morali kubwa ya kujituma na kujitolea uwanjani kwa ajili ya timu tofauti na Simba. Haiwezekani Simba akikosekana mtu mmoja au wawili basi timu inakuwa haichezi vizuri au haipati ushindi inavyotakikana,” alisema Sued na kuongeza;

“Tatizo la Simba ina wachezaji wazuri ila hawajitoi kwa asilimia zote na ndicho kinachowaponza.”

Sued alisema viongozi waingie mfukoni na kusajili wachezaji katika nafasi tatu muhimu ambazo zimeonekana kulega lega ili kuimarisha timu hiyo kama inataka kutimiza malengo yake.

“Kuna nafasi kama tatu hivi wanatakiwa waongezwe watu, kwanza apatikane kiungo mchezeshaji asilia maana tangu alivyoondoka Rally Bwalya timu haina kiungo mchezeshaji.

“Wakati mwingine anatumika Clatous Chama lakini asipokuwepo ndio unaona timu inayumba, sasa hilo ni tatizo ni tofauti na Yanga ina viungo wazuri wachezeshaji kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Salum Abubakary ‘Sure Boy’,” alisema Sued na kuongeza;

“Pia atafutwe mshambuliaji wa maana wa kucheza pacha na Phiri kwani phiri anapewa majukumu makubwa hadi wakati mwingine yanamchosha kwani haiwezekani ahangaike mwenyewe atafute mpira ndio aende akafunge sasa hadi akilifikia goli si amechoka.

“Wale washambuliaji waliopo naweza kusema hawaendani na kasi ya Phiri ndio maana hata akipangwa nao anakuwa anapata shida kwani yeye ana kasi sana wenzake wako taratibu.

Sued alisema inatakiwa kusajili beki wa kushoto wa kumsaidia Mohammed Husein’ Tshabalala’.

“Gadiel ni mchezaji mzuri ila kaachwa mbali sana kwa ubora na Tshabalala hivyo nafasi hiyo lazima ipate mtu kazi hasa kwani kwenye beki wa kulia hakuna tatizo, Kapombe yuko vizuri na hata yule dogo ambaye ni mbadala wakle Israel Mwenda anakwenda vizuri waendelee kumpa mechi ili kuzidi kumjengea kujiamini,” alisema Sued.